Wa uongo mwanamme, asiliye ufisadi,
Huutaliki udume, imani akaritadi,
Akabakia mahame, na maghofu ya fuadi,
Mwanamme wa uongo, ufisadi asiliye!
Mwiliwe ndiyo kaziye, na moyowe maabadi,
Sio aridhikaye, daima ana nakidi,
Kesho si afikiriaye, wala si mtunza ahadi,
Mwanamme wa uongo, ibada yake ni ngono!
Mme huyu wa nazaa, asiliye kukaidi,
Kila siku hungojea, anapoliwa na Idi,
Siye mwenye kutulia, asili kutaradadi,
Wanaozuka janibu, ujira wao zawadi,
Na wnaokuwa ghaibu, jivu lao makusudi,
Hadhara huja kujibu, ipayukapo mihadi,
Mwanamme wa uongo, ufisadi asiliye!
Huipamia nasibu, wakaona ni juhudi,
Wakaiweka kwa ghibu, yasiyokuwa ni sudi,
Na mitende ya adhabu, ikaja kuwafaidi,
Mwanamme wa uongo, ibada yake ni ngono!
Hana muda kwangalia, mateso waogeleao,
Kiburi chake hukwea, kuitani taabu zao,
Hali kwa asilimia, ni ndani ya uwezo wao,
Mwanamme wa uongo, ufisadi asiliye!
Kila wanachokigusa, budi kuvuta nuksi,
Kila wanachokinusa, hutapakaa mikosi,
Wadudi kutomtakasa, wote wakawa kamasi,
Mwanamme wa uongo, ibada yake ni ngono!
Huja wakanyofolewa, kwenye uongo wazua,
Roho kwenda kutupiwa, Bahari tusizojua,
Mfu wakabakia, huku washughulikiwa,
Mwanamme wa uongo, ufisadi asiliye!
Jabari kumwelekea, zitapungua balaa,
Vingine tutapokuwa, tutazidi kuumia,
Fursa ameshaitoa, tawba kuililia,
Mwanamme wa uongo, ibada yake ni ngono!
No comments:
Post a Comment