HABARI nimesikia, kuwa wa fedha vichaa,
Wameishajilimbikia, eti sasa wazimwaa,
Kusudi na yao nia, hakuna anayejua,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Kwa wingi zilivyojaa, kila mtu agawiwa,
Hakuna wa kuchagua, wote kwao abiria,
Lengo sijalitambua, nabakia kushangaa,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Punda ingelikuwa, ngejuwa wamelemewa,
Mwenye punda achezewa, na dhihaka kufanyiwa,
Mtoni akajitia, chumvi
maji kwenda kuwa,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Na wanaokusudiwa, kura wanaoshikilia,
Vyamani walimokuwa, waziwazi ni bidhaa,
Bei imeshaamuliwa, taslimu wanatoa,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Karuni ninayemjua, japo wingi ulimzidia,
Bure kitu hakutoa, hadi alipofukiwa,
Hawa sijawaelewa, gia gani watumia?
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Nyumbani wazichukua, ugenini kufukia,
Kisha wanajichengua, na mikwara kujitia,
Ukiona yaelea, juwa wameazimia,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Matofali wachukua, dhahabu yaliyokuwa,
Kaziye si kujengea, ila kuji9nyeshea,
Ukubwa uliokuwa, hasara kwenye dunia,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Wanywa hadi kujinywea, ibilisi kakolea,
Hio waalofurahia, Mola hajafurahia,
Kicheko kilichokuwa, kilio kakitohoa,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Milma waelemea, bondeni kulikouwa,
Huku juu umejaa, chini wazidi kupyway,
Na bado twatarajia,
kisiwa tutabakia ?
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Kama pombe ingekuwa, sababu ningeijua,
Wataka watu kulewa, ovyo wakajisemea,
Kisha lao wakalitwaa, pasina wao kujua,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Keki ingelikuwa, kwenye basi imekuwa,
Kisha dawa imetiwa, shabaha ningegundua,
Wanuia abiria, kwenda mbele waibia,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Mimi hili sijajua, la tajiri kuwa na njaa,
Ikawa yamelvyaa, hadi chini twamzoa,
Kuna kitu sijajua, bado nakiangalia,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Si wa bure ukichaa, ovyoovyo kuzigawa,
Kuna sababu na nia, ila sijaigundua,
Kofia nitaivua, kija mtu kunambia,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Semeni Watanzania, haya mnayoyajua,
Vimbgwanga vyakaribia, mengi tutashuhdia,
Watu nguo watavua, sapoti kwenda kutoa,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
Ni wakati wa maridhia, watu kuyafikiria,
Akili wakatumiwa, si kwa moyo kuzainiwa,
Kisha wakaja kuyajutia, siku wasioitambua,
Kuna vichaa wa fedha, msijekuwachagua !
No comments:
Post a Comment