Monday, October 14, 2013
N Y E R E R E DEI 2013
Bismillahi Jalia, mmiliki wa dunia,
Mbingu na sayari pia, tujuazo, tusojua,
Yahillahi mtambua, msafi pasipungukiwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Peke wa kuabudiwa, aidha wa kutegemewa,
Mshiriki usiyekuwa, japo wakusingizia,
Daraja unayejua, waja za kuwapatia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Laiti ungelikuwa, haya ningekushtakia,
Nchini yanayoingia, na macho twayafungia,
Nchi uliowaachia, weye ungewashangaa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Ibilisi katuvaa, twaiabudu dunia,
Watu miungu wakawa, na ibada kufanziwa,
Wa kutusamehea, hawezi mwingine kuwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Ufahari wamejaa, nchi uliowachia,
Matumizi watumia, tajiri utadhania,
Washindwa kuvipangia, fakiri kutunasua,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Hekalu wajijengea, matembe tunakalia,
Na manyatta ndio njia, Umasaini sikia,
Ila kuna walojaliwa, vya milioni kuvaa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Nyumba wanatuvunjia, wala si kutujengea,
Mali aisli yatumiwa, ughali kutwongezea,
Nusura h atuaijua, japo tumeahidiwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Ibada wasiojua, migongano wanazua,
Kuchinja ulichinjiwa, na Islamu alokuwa,
Vipi wawakatalia, au visa wanavizua ?
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Udini unaingia, manabii twajaliwa,
Cheo wanajinyanyua, na njia kufaragua,
Wakuu wakawaambia, kifalme kujiishia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Elimu twaichezea, kifaurongo ikawa,
Watasi wanakamia, wa kwao kupendelewa,
Hatarini kuigawa, nchi ulotuachia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Maji yazidi potea, na tenda zinaongea,
Masikini wafulia, walonacho kwogelea,
Shilingi yazidi kupaa, mwezini itafikia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Umeme sasa nazaa, tayari imeshakuwa,
Mashamba wajilimia, Kwa ya Mtera kumwaa,
Mengi tusiyoyajua, nani aatatuambia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Amoeba imekua, tatizo linalojizaa,
Ngomba inavyozidi kulia, viraka twaongezewa,
Nafuu inatukimbia, kilio kimebakia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Udugu wajifufua, macho tunaufumbia,
Wakubwa inapokuwa, hatuna la kuongea,
Kisirani inakuwa, wazidi kujichimbia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Vyama vimeingiliwa, na hasidi na nazaa,
Vyao wanajifanzia, wapendalo huamua,
Waviza demokrasia, ya kwao kufanikiwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
makundi
Yabanwa demokrasia, na ndondocha walokuwa,
Vyumbani waliotiwa, misumari kupigiliwa,
Kisha kwa kukosa hewa, weupe hugeukia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Ukabila wa siasa, nchini umeshaingia,
Wachache wajiteua, ya wengi wakafukia,
Anayejifaragua, uhaini atatiwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Ukubwa twauchukua, ila maendo yavia,
Nyuma vile twarejea, kilichopo kupotea,
Upya tunayaanzia, hata yaliyotangulia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Ufisadi umetua, nani aje kuung'oa,
Manake una wafaa, wajuao wanajua,
Kulalama sijajua, mabomu nayahofia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Twatakiwa kunyamaa, ukweli kuufukia,
Kulaumu si sheria, hakiye yachukuliwa,
Twatakiwa vumilia, lolote tukitendewa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Maguvu sasa ni njia, wenye nayo watumia,
Fedha nayo sasa pia, imeshapewa sheria,
Kama nayo sipokuwa, haki inanunuliwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Madini yachimbuliwa, hata na gesi nayo pia,
Swali lisilojibiwa, hivi nani kumfaa,
Ni wengi itajakuwa, au ndugu na jamaa?
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Twahofia kutokea, kama kule Nigeria,
Na JIneikwatoria, ambako zabanjuliwa,
Wakuu wakaogelea, hadi wa chini wafulia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Wazawa wasimuliwa, thamani yaondolewa,
Maisha juu yapaa, hali chini wadumaa,
Wataipataje furaha, inashangaa dunia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Imani zimeachiwa, mikingamo kuingia,
Wa chini juu akawa, ya wengine kuamua,
Ndio wakajisemea, ya wakuu wasokuwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Mengi waliahidiwa, dirishani yatokea,
Mlangoni yazuiwa, ngangari yanashupaa,
Musuli zikishakuwa, za akili kutanua,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Mipango twaihofia, kinyume yakaakaa,
Ya mbele yanakosewa, ya nyuma yakafatia,
Kipaumbele chavia, shamba na mjini pia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Si vyema haijawa, mikakati Tanzania,
Mifumo tunafumua, badala kujishonea,
Watu wajiamlia, jinsi wanavyosikia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Uimla twauzua, utakuja tuumbua,
Na kwenye hii dunia, tuishio kwa kupaa,
Yallahi twakulilia, baa kutuepushia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Vijiji vinadumaa, vile ulivyotuachia,
Laiti ungerejea, Mwalimu ungeshangaa,
Maktaimu vinatia, na watu washangilia ?
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Kinamama wanalia, shamba wanasahauliwa,
Wateta wawanyapaa, wa mjini wanabebwa,
Wataacha nyong'onyea, na uzee kuingia ?
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Mshairi achukiwa, kwenye yako Tanzania,
Sasa wamnyanyapaa, kwa uongo kukataa,
Kweli akapigania, watu macho kufungua,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Maisha yetu ya jaa, uleo yamechelewa,
Wanayoyafikiria, sio yanayotakiwa,
Na wanayoyaamua, tafiti zake ukiwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Arijojo imekuwa, mengi yanajiendea,
Ila inapokuwa, maandamano kung'oa,
Na machinga kusanzuliwa, na vyao vikaharibiwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Hoi demokrasia, dripu imeekewa,
Spitali yatibiwa, unyafuzi wazidia,
Katibani kuingia, mengi sana yapunguwa,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Katiba twaililia, mbali ikatuchukua,
Tusiwe wa kudumaa, kwa uoga kutwingia,
Mola tunokusudia, yote ungeyajalia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Wachache wapigania, ya kwao kufanikiwa,
Ya wengine kutibua, kwa nguvu au ridhaa,
Hatari twajionea, ujanja ukizidia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Latifu mhimidiwa, ipokee yangu dua,
Batili kuiondoa, ya haki yakabakia,
Haramu kuicheua, halali ikasalia,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
Tamati nimefikia, mbele sintoendelea,
Miye kusahauliwa, ni haki nimeridhia,
Ila ninayowambia, haya mngeyachukua,
Zimebaki kumbukumbu, Nyerere Dei yapita !
makillla
Nyerere Dei, 2013.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment