Watu wanapoumia, kwayo kiu nayo njaa,
Huku jua lapaua, kichwani kilichokuwa,
Kisha wazidi udhia, wema kutojionea,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Nchi wanapopakua, kama yao vile kuwa,
Vitamu wakajilia, na akibani kutia,
Huruma ikapotea, roho mbaya ikakua,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Cha wengi kinapoliwa, mmoja kujishibia,
Haya ikendaugua, na 'spitali kutibiwa,
Na aibu kulemaa, ukabakia ukiwa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Maji yanapopotea, dhahabu nayo yakawa,
Watu wakajisifia, ya msingi kujaliwa,
Kicheko wakaangua, raia wakifulia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Maji wanapokataa, muhimu hayajakuwa,
Hesabu yakatungiwa, kasoro yaliyokuwa,
Kifanzwacho kisokuwa, zikaingia sanaa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Giza wa kijivunia, na nuru kuikataa,
Kwa hadaa kuzidiwa, kiatu kugeuziwa,
Huwashangaa dunia, mgongo kuwaachia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Elimu ikivuliwa, nguo iliyoivaa,
Matambara ikapewa, na bomba za kuchakaa,
Maji zisizoyatoa, ila kelele na hewa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Mengi huyafikiria, ya ufakiri na njaa,
Sahaba kuwafukua, na hekima ilokuwa,
Ukweli nikaujua, yao na Islamiya,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Wao ndio watwabia, kilimo kwanza ni dawa,
Kumbe njia watumia, kinyume zilizokuwa,
Na sasa twajionea, shere yanatuchezea,
Heri fakiri ukawa, wa mali kwenye dunia,
Lulu waweza ivua, mara tajiri ukawa,
Dunia ikakujua, nawe uliipitia,
Heri fakiri ukawa, wa elimu kutokuwa,
Wengine watakufaa,za kwako ukajitia,
Nawe ukatumia, uweze kujichumia,
Ila ni kubwa balaa, fakiri wewe ukiwa,
Uongozi kuishiwa, ufakiri ukavaa,
Haitokufaa daawa, kila kitu hufulia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Hufulia ya kufaa, iwe jalala na jaa,
Dhahabu ukiipewa, chini utaichimbia,
Au bahati ikiwa, bure wewe utagawa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Fakiri wa kuongoa, ndio mama wake njaa,
Nchi yote huishiwa, ombaomba kubakiwa,
Hata wakajisifia, uongo unabakia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Uongo ukazaliwa, kwa uongozi wa njaa,
Watu wakapakuliwa, maneno yaliyoyaa,
Kitu yasiyokujakuwa, ila kuongeza makiwa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Hudai kuendelea, na watu walala njaa,
Takwimu hutapikiwa, zinazonuka hadaa,
Hali ukiangalia, ubaki jisikitikia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Vipimo hujiokotea, dampo vilivyotupiwa,
Hadharani kutumia, aibu vilivyojaa,
Watu wakakebehiwa, na ukweli wasojua,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Njaa mama wa balaa, mlango twamfungulia,
Na huku twajiendea, kama kitu haijawa,
Lusifa afurahia, mavuno mengi yakawa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
No comments:
Post a Comment