Saturday, November 10, 2012

WAKOMA MWABAKI NAO ?

 TABIA akigundua, kuonya kaamriwa,
Mwapasa kuyasikia, kutengwa budi ikawa,
Kati mkiwaachia, wengine wataugua,
Wakoma  huwa watengwa, kuyaepuka madhara !

Rushwa tumeitambua, ni ukoma waingia,
Kimya tukijikalia, itakuja tuumbua,
Umma naushadidia,  hili kuja lihofia,
Wakoma huwa watengwa, kuiepuka hasara !

Kut9jua nakataa, hilo haliwezi kuwa,
Huruma tumeingia, utadhani ni ukiwa,
Macho tunalifumbia, liletalo kulemaa?
Wakoma  huwa watengwa, kuyaepuka madhara !

Tunatia ujamaa, na udugu kutetea,
Karibu tunawajua, pembeni hawajakaa,
Tutumialo sinia, hilohilo watumia,
Wakoma huwa watengwa, kuiepuka hasara !

Lawama tukizitoa, nini zinasaidia,
Au aibu na  haya, huwa hapo zapotea,
Na katika  jumuiya, ndo pekee walokuwa ?
Wakoma  huwa watengwa, kuyaepuka madhara !

Kuna mengine udhia, mtu ukifikiria,
Mafuu utadhania, jinsi tunavyoamua,
Au kama twachezewa, kutogwa na wasiokuwa,
Wakoma huwa watengwa, kuiepuka hasara !

Mizizi tunaing'oa, kwa majani twapandia ?
Mbuyu haijakuwa, watu kuja kushangaa,
Watauona mzaha, wakacheka na kulia,
Wakoma  huwa watengwa, kuyaepuka madhara !

Ujumbe umetimia, imebaki kuamua,
Salama kutopotea, Tanzania wangojea,
Maamuzi kusikia, ulua yaliyojaa,
Wakoma huwa watengwa, kuiepuka hasara !

No comments: