Saturday, November 10, 2012

Treni bila dereva

 Muongoza bila kuwa, garimoshi hupwelea,
Watu likawatishia, nje, ndani walokuwa,
Usalama hupotea, maafa mkahofia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Na ndani unapokaa, budi kutazama njia,
 Wapi mnaelekea, na kama salama yawa,
Vingine inapokuwa, breki ukazitia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Treni bila dereva, lazima kuacha njia !
Kona ukazitambua, na harari zilokuwa,
Ovyoovyo kijiendea, watu utaparamia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Vilima usipojua,na mteremko ya njia,
Huangusha mabehewa, kilio kikubwa kuwa,
Vyuma vikajichimbia, na vingi kujipindia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Dereva anatakiwa, chombo kukihudumia,
Njiani kujipitia, wote salama wakawa,
Vingine inapokuwa, uhai twauchezea,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Wapo wakudandia, na rafiki walokuwa,
Usije kuwaachia, bure wakajipandia,
Au za hongo wakanunua, tiketi zio bandia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Hasara utaingia, shirika kuja jifia,
Kitambo ukiridhia, milele hudidimia,
Dunia hutuchezea, mitihani tulopewa,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Mawasiliano kivia, vingine hautajua,
Nyingine weza ingia, kwa mambo ya kusikia,
Hatari kubwa ikawa,kwa maisha na rupia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Dereva atarajiwa, kazi moja kuifaa,
Nyingine akichukua, anaweza kuzidiwa,
Kija kutahamakia, mkenge mmeingia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Safari yaashiria, dereva hatujamjua,
Na treni yakimbia, breki haijatiwa,
Sisi tunaposhangaa, wengine wachekelea ?
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

No comments: