Thursday, January 26, 2012

Yuraniamu Tanzania hapana...


I hate Uranium, marauders spare my people

1.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Nchi inayolaaniwa,
Maajabu huamua,
Wizi wakishaujua,
Lolote watajifanyia,
Huongozwa na tamaa,
na mwisho sote twajua:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

2.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Bungeni ukiangalia,
Watu wengi wasinzia,
Hawa ndio Watanzania,
Dhamana mtawaachia
Mengi wanayoamua,
kichefuchefu yatia:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

3.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Wabunge wa kutegemewa,
Hofu sasa wanatutia,
Si wate wa kufikiria,
Bali ndiyo kuitikia,
Maamuzi yenye udhia,
Rahisi sana kuua:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

4.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Ni wavivu waliokuwa
Vigumu kujisomea
Miswaada kuipitia
Sio linalotarajiwa
Bungeni mbumbumbu wawa:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

5.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Marekani wakataa,
Makwao kuichimbua,
Kondomu na vyandarua
Sisi tukishapatiwa
Hili tunalikubalia?
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

6.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Katazameni dunia,
Kwingineko kulokuwa,
Yuraniamu inaua
Na ulemavu kusia
Viumbe wanazaliwa
Ajabu waliokuwa:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

6.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Ni heri kilema kuwa
Wa mwili unaovia,
Kuliko kilema kuwa
Wa akili kutumiwa
Na wazungu wenye njaa
Uhai wasiotutakia:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

7.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Ubepari wakolea,
Chamani unaenea
Wajamaa walokuwa
Uuaji wanadhamiria
Hakika nitawashangaa,
Yao mkiyasikia:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

8.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Uranium balaa
Tuepuke kukaribia
Vipo tulivyojaliwa
Havifai kuvifukua
Ni mizimu iliyokuwa
Ukishika walipuliwa:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

9.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Bado hatujafikia
Kuwa nayo kali njaa
Kama yao waheshimiwa
Ubinafsi walojaa
Mwenye njaa wasomjua
Mzigo wanaokuwa
Kwa nchi kutokuifaa:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

10.
Laana twawaombea, waidhinishao hili,
kuchimbwa Uranium, hapa kwetu Tanzania,
Wakati haujafikia, na hatujajiandaa,
ha hatunavyo vifaa, tahadhari kuchukua:
Hakimu twamgeukia
Mmiliki wa dunia
Haya tutamuachia
Uamuzi kufikia
Na tishio wanaokuwa
Kuhukumu linalofaa:
Uchu na zenu tamaa, tunawaonya wakubwa,
mauti mwatutakia!

Please Lord protect the ignorasmuses!


Saturday, January 7, 2012

Njaa haina adabu

Njaa kali mtihani, kwa mja mjaribiwa,
Hata vyake vya thamani, kwa watu atavitoa,
Moyoni na akilini, muflisi kuishia,
Njaa haina adabu, hata mkubwa huuzwa!

Huukosa umakini, subira kuwapotea,
Kingine wasiamini, ila kilicho kutwaa,
Rahisi kuwazaini, wafate za mkato njia,
Njaa haina adabu, hata mpenzi huuzwa!

Huwa hawajiamini, wala Mola kumjua,
Wao wenyewe hudhani, wanaweza kuwa dawa,
Aya hawazibaini, zizungumziayo haya,
Njaa haina adabu, hata mzazi huuzwa!

Hawa watu wa zamani, ukale umewavaa,
Ukafiri yao dini, japo majina wapewa,
Ukiona yaundani, ukweli huwatambua,
Njaa haina adabu, hata mtoto huuzwa!

Njaa inawarubuni, maovu kukimbilia,
Na wakishakuyawini, wanaingia hatia,
Wakawa ni mashakani, sikuzote wanalia,
Njaa haina adabu, hata mkubwa huuzwa!

Hujuta wasiamini, mambo waliyoyazua,
Huona kama utani, hata watu wakiua,
Huwakumba mashetani, kwa yao kuwatumia,
Njaa haina adabu, hata mpenzi huuzwa!

Majuto wakisaini, mjukuu yanakuwa,
Kazi kupata auni, na rehani kuitwaa,
Huyoyoma tumaini, giza chele kubakia,
Njaa haina adabu, hata mzazi huuzwa!

Mtunzi simuamini, kila aliye na njaa,
Hutumia darubini, yake yote kwangalia,
Nikishakuyabaini, nafasi nitamwachia,
Njaa haina adabu, hata kilema huuzwa!

Kabla siiamini, baada sijaijua,
Huishia hatarini, kwa huruma kujitia,
Na wabaya duniani, hili wanalitumia,
Njaa haina adabu, hata tajiri huuzwa!

Ujinga kama mtaji

Ni wazuri watungaji, wa mateso ya kutojua,
Kwao hili wanahiji, magoli kujifungia,
Kisiasa wazidi waongo kuaminiwa,
Ujinga kama mtaji, wawekeza watawala!

Hukuridhisha kwa uji, wakatumia maziwa,
Uongo hukufariji, milioni wakatwaa,
Hakuna wa kuwahoji, hukumu waitania,
Ujinga kama mtaji, watumia watawala!

Sio watu wa Buruji, akili zimefubaa,
Hata wakiwa majaji, wengine huwatumia,
Yakavia mataraji, na ndoto kuenguliwa,
Ujinga kama mtaji, wauenzi watawala!

Vyateketea vijiji, kwa ujinga kuachiwa,
Hawana la kuwahoji, wakubwa waliokuwa,
Kuna wakubwa wa jiji, siasa zawatetea,
Ujinga kama mtaji, wawekeza watawala!

Huwa hawanayo maji, kwenda nayo watishiwa,
Husema jema haliji, wengine wakichaguliwa,
Ila wao wana mji, ukubwa wamejaliwa,
Ujinga kama mtaji, watumia watawala!

Waoga wanavijiji, kila ukiwatishia,
Huzimika yao chaji, simu zikawa kimya,
Ukabakia ulaji, pasipo kusumbuliwa,
Ujinga kama mtaji, wauenzi watawala!

Tofauti na wanamji, macho wameyafungua,
Kila kitu hukuhoji, ukweli kuuchimbua,
Kisha wazuri walaji, hula chako wakaambaa,
Ujinga kama mtaji, wawekeza watawala!

Utawala kutaraji, wajinga kujivunia,
Senti ukiwafariji, kura watakuachia,
Utawale mwanamji, matunda kujichumia,
Ujinga kama mtaji, watumia watawala!

Chama chenye wajuaji, hapa ngoma huchezea,
Wakaukata mtaji, na utumwa kuondoa,
Upinzani wende hiji, na uhuru kuujua,
Ujinga kama mtaji, wauenzi watawala!

Muua demokrasia, si rafiki wa mwananchi!

WAFUASI wenye njaa, chama wanapokimbia,
Kwa mkubwa kuwanunua,kwingine anayetokea,
Wananchi bora kujua,demokrasia huua,
Muua demokrasia, si rafiki wa mwananchi!

Ukiritimba azua, uzidi kutusumbua,
Ubora unaovia, na nchi ikapotea,
Tuonekane vichaa, katika hii dunia,
Muua demokrasia, si rafiki wa mwananchi!

Hii ni hovyo ruia, wangapi kuwanunua?
Wenyewe watuibia, kisha wanatununua?
Naona tumeshapagawa, kama tunayavumilia,
Muua demokrasia, si rafiki wa mwananchi!

Ushindani watakiwa, mambo yetu bora kuwa,
Huyo anayekataa, udhaifu artwachia,
Kila tunapokomaa, mkengeni huishia,
Muua demokrasia, si rafiki wa mwananchi!

Tabasamu la kuua

Mwanamwali kajaliwa, tabasamu la kuua,
Kila ukimuangalia, hutaka msogelea,
Uzuri ukaujua, na tabasamu kupewa,
Wengi unawahadaa!

Mwanya ukiufungua, mioyo huugulia,
Meno ukiyakwanyua, ni vito huvidhania,
Kila mtu huwania, wa kwanza kuyachukua,
Wengi unawahadaa!

Ulimi ukiutoa, mwili husisimuliwa,
Kidani hukidhania, chekundu kilichokuwa,
Mikono huinyanyua, kutaka kukipokea,
Wengi unawahadaa!

Mashavu yakibonyea, na mashimo kutokea,
Hutamani kuingia, milele kujahamia,
Kwingine kutotembea, hata milele ikiwa,
Wengi unawahadaa!

Sauti ukiitoa, wimbo mweama unakua,
Tabasamu ukatia, watu huchanganyikiwa,
Kila mwenye yake hawa, haachi kukuangalia,
Wengi unawahadaa!

Piganeni na nafsi

NAFSI hupigania, yenyewe kutambuliwa,
Haina katu wasaa, kwa yake yasiyofaa,
Hutaka jiangalia, juu zaidi ikawa,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Nayo ukiiachia, hakika utapotea,
Mabaya huyachukua, bora ikayadhania,
Na mitaa isofaa, ikawa ni yake njia,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Mali huikimbilia, hata haramu ikiwa,
Ukuu kujipatia, ipate kuheshimiwa,
Fukara huwakimbia, hasara kutoingia,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Ila wanaojitambua, kudhibiti wanajua,
Ubinadamu huvia, wengine ukikimbia,
Na utu hujatimia, kwa wengine kuwafaa,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Shetani hukuzuia, mazuri kuyatanzua,
Ukaishia balaa, mashauzi na nazaa,
Umri ukapotea, kwa mengi yasiyofaa,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Na wanaoelekea, huko hawatoingia,
Wataka salama njia, kwa akhera na dunia,
Ibada huitambua, nafsi kuisaidia,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Hakika wanaojua, nafsi huizuia,
Kisha kuishikilia, ovyo kutokukimbia,
Isije ikayavaa, mtu yasiyomfaa,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Nafsi nakulilia, achana nayo mabaya,
Hapa ulipo tulia, mazuri kukuchagulia,
Na malaika wakawa, rafiki wa kuteua,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!