Saturday, January 7, 2012

Piganeni na nafsi

NAFSI hupigania, yenyewe kutambuliwa,
Haina katu wasaa, kwa yake yasiyofaa,
Hutaka jiangalia, juu zaidi ikawa,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Nayo ukiiachia, hakika utapotea,
Mabaya huyachukua, bora ikayadhania,
Na mitaa isofaa, ikawa ni yake njia,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Mali huikimbilia, hata haramu ikiwa,
Ukuu kujipatia, ipate kuheshimiwa,
Fukara huwakimbia, hasara kutoingia,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Ila wanaojitambua, kudhibiti wanajua,
Ubinadamu huvia, wengine ukikimbia,
Na utu hujatimia, kwa wengine kuwafaa,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Shetani hukuzuia, mazuri kuyatanzua,
Ukaishia balaa, mashauzi na nazaa,
Umri ukapotea, kwa mengi yasiyofaa,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Na wanaoelekea, huko hawatoingia,
Wataka salama njia, kwa akhera na dunia,
Ibada huitambua, nafsi kuisaidia,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Hakika wanaojua, nafsi huizuia,
Kisha kuishikilia, ovyo kutokukimbia,
Isije ikayavaa, mtu yasiyomfaa,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

Nafsi nakulilia, achana nayo mabaya,
Hapa ulipo tulia, mazuri kukuchagulia,
Na malaika wakawa, rafiki wa kuteua,
Piganeni na nafsi, wengine kujawafaa!

No comments: