Mwanamwali kajaliwa, tabasamu la kuua,
Kila ukimuangalia, hutaka msogelea,
Uzuri ukaujua, na tabasamu kupewa,
Wengi unawahadaa!
Mwanya ukiufungua, mioyo huugulia,
Meno ukiyakwanyua, ni vito huvidhania,
Kila mtu huwania, wa kwanza kuyachukua,
Wengi unawahadaa!
Ulimi ukiutoa, mwili husisimuliwa,
Kidani hukidhania, chekundu kilichokuwa,
Mikono huinyanyua, kutaka kukipokea,
Wengi unawahadaa!
Mashavu yakibonyea, na mashimo kutokea,
Hutamani kuingia, milele kujahamia,
Kwingine kutotembea, hata milele ikiwa,
Wengi unawahadaa!
Sauti ukiitoa, wimbo mweama unakua,
Tabasamu ukatia, watu huchanganyikiwa,
Kila mwenye yake hawa, haachi kukuangalia,
Wengi unawahadaa!
Saturday, January 7, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment