Ni wazuri watungaji, wa mateso ya kutojua,
Kwao hili wanahiji, magoli kujifungia,
Kisiasa wazidi waongo kuaminiwa,
Ujinga kama mtaji, wawekeza watawala!
Hukuridhisha kwa uji, wakatumia maziwa,
Uongo hukufariji, milioni wakatwaa,
Hakuna wa kuwahoji, hukumu waitania,
Ujinga kama mtaji, watumia watawala!
Sio watu wa Buruji, akili zimefubaa,
Hata wakiwa majaji, wengine huwatumia,
Yakavia mataraji, na ndoto kuenguliwa,
Ujinga kama mtaji, wauenzi watawala!
Vyateketea vijiji, kwa ujinga kuachiwa,
Hawana la kuwahoji, wakubwa waliokuwa,
Kuna wakubwa wa jiji, siasa zawatetea,
Ujinga kama mtaji, wawekeza watawala!
Huwa hawanayo maji, kwenda nayo watishiwa,
Husema jema haliji, wengine wakichaguliwa,
Ila wao wana mji, ukubwa wamejaliwa,
Ujinga kama mtaji, watumia watawala!
Waoga wanavijiji, kila ukiwatishia,
Huzimika yao chaji, simu zikawa kimya,
Ukabakia ulaji, pasipo kusumbuliwa,
Ujinga kama mtaji, wauenzi watawala!
Tofauti na wanamji, macho wameyafungua,
Kila kitu hukuhoji, ukweli kuuchimbua,
Kisha wazuri walaji, hula chako wakaambaa,
Ujinga kama mtaji, wawekeza watawala!
Utawala kutaraji, wajinga kujivunia,
Senti ukiwafariji, kura watakuachia,
Utawale mwanamji, matunda kujichumia,
Ujinga kama mtaji, watumia watawala!
Chama chenye wajuaji, hapa ngoma huchezea,
Wakaukata mtaji, na utumwa kuondoa,
Upinzani wende hiji, na uhuru kuujua,
Ujinga kama mtaji, wauenzi watawala!
Saturday, January 7, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment