Njaa kali mtihani, kwa mja mjaribiwa,
Hata vyake vya thamani, kwa watu atavitoa,
Moyoni na akilini, muflisi kuishia,
Njaa haina adabu, hata mkubwa huuzwa!
Huukosa umakini, subira kuwapotea,
Kingine wasiamini, ila kilicho kutwaa,
Rahisi kuwazaini, wafate za mkato njia,
Njaa haina adabu, hata mpenzi huuzwa!
Huwa hawajiamini, wala Mola kumjua,
Wao wenyewe hudhani, wanaweza kuwa dawa,
Aya hawazibaini, zizungumziayo haya,
Njaa haina adabu, hata mzazi huuzwa!
Hawa watu wa zamani, ukale umewavaa,
Ukafiri yao dini, japo majina wapewa,
Ukiona yaundani, ukweli huwatambua,
Njaa haina adabu, hata mtoto huuzwa!
Njaa inawarubuni, maovu kukimbilia,
Na wakishakuyawini, wanaingia hatia,
Wakawa ni mashakani, sikuzote wanalia,
Njaa haina adabu, hata mkubwa huuzwa!
Hujuta wasiamini, mambo waliyoyazua,
Huona kama utani, hata watu wakiua,
Huwakumba mashetani, kwa yao kuwatumia,
Njaa haina adabu, hata mpenzi huuzwa!
Majuto wakisaini, mjukuu yanakuwa,
Kazi kupata auni, na rehani kuitwaa,
Huyoyoma tumaini, giza chele kubakia,
Njaa haina adabu, hata mzazi huuzwa!
Mtunzi simuamini, kila aliye na njaa,
Hutumia darubini, yake yote kwangalia,
Nikishakuyabaini, nafasi nitamwachia,
Njaa haina adabu, hata kilema huuzwa!
Kabla siiamini, baada sijaijua,
Huishia hatarini, kwa huruma kujitia,
Na wabaya duniani, hili wanalitumia,
Njaa haina adabu, hata tajiri huuzwa!
Saturday, January 7, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment