Thursday, June 21, 2012

Nikipendacho si mwili

Nikipendacho mpenzi, ni roho na moyo wako,
Sio mwili wala ngozi,  huisha kwenye maziko,
Viwili hivyo vya enzi, hata huko niendako,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Ni roho na moyo wako, nikipendacho si  mwili,
Na katika uhai wako, hivyo kwangu ndio mali,
Na mimi kila niliko, njema hutakia hali,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Nikipendacho ulimi, usiokuwa muhali,
Daima unaojihami, kutotia idhilali,
Ukataao rasmi, umbeye kuuhimili,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Nipendacho adili, maovu haufumi,
Ukawa kwangu kandili, na ndia yangu ya lami,
Mitego kuikabili, kwangu ukawa ami,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Na roho niipendayo, makuu isiyokuwa,
Heshima ujengayo, bila ya kulaumiwa,
Tamaa isiyo nayo, haliye unaridhia,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Roho isiyo kinyaa, na matapishi kujaa,
Ndani inayotulia, yangu kunihudumia,
Mola inayomhofia, mabaya ikakimbia,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Mema ilodhamiria, kwa mchana na usiku,
Machozi inayotoa, uchamungu na shauku,
Inayowasaidia, walo kule, walo huku,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Moyo ninaoutaka, ovyo usiotamani,
Ujajuayo mashaka, ya uchu wa duniani,
Kila siku huridhika, kipatacho mkononi,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Kwa mwili tunaponzeka, usizo nazo akili,
Watu tukadangayika, wengi tukawa anzali,
Mitihani kuanguka, tuwe daima twafeli,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Mwili mkubwa ajali, bure unathaminiwa,
Hata usio akili, na udhaifu kujaa,
Wenye giza si kandili, mushiriki ulokuwa,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Rijali na wanawali, mwishowe  wakaanguka,
Zidhoofu zao hali, yakawafika mashaka,
Pasiwe na afadhali, iwe vuta na chanika,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Waweza upenda mwili, mtu akose akili,
Na rijali na wanawali, kizazio bilkuli,
Kikawa chote muhali, kujaliwa ya akili,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Nenda kaoe akili, nakushauri bilali,
Mwili ni kitu muhali, uitakapo akili,
Ni mkubwa ubahili, bongo kwake ni ajali,
Nikipendacho si mwili, ni roho na moyo wako !

Mganga hadai mchicha

Mchicha hadai mganga, lakini hudai kuku,
Maombi akiyachonga, si ya mia ni ya buku,
Hata  akiwa ni mwanga, ajua hili si huku,
Mganga haagizi tui, aagizacho ni nazi !

Na katu hatojivunga, eti akadai yai,
Ila kama la kuroga, viza lisilostahi,
Kamuone akimwaga,  ni maji wala si chai,
Mganga haagizi tui, aagizacho ni nazi !

Mganga haombi kaniki, ila khanga na baibui,
Tena ni ya urafiki, si Mchina hajawahi,
Mengine hashughuliki, kwa kitenge hufurahi,
Mganga haagizi tui, aagizacho ni nazi !

Mganga haombi hela, mizuka watakuomba,
Faraji sio farijala, kama maziwa akiomba,
Haombi kama ya kula, ni ya  simba ataomba,
Mganga haagizi tui, aagizacho ni nazi !

Monday, June 18, 2012

Ghorofa haina msingi

VIJANA wanaondoka, wazee wamewachoka,
Kisa wanahamanika, ukale unatukuka,
Na nchi wanaoshika, hawataki badilika,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Msingi umeng'oleka, wa vijana watukuka,
Vibabu vyahangaika, upepo kuzuilika,
Kwao makubwa mashaka, hawana lenye hakika,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Mafuriko yamezuka, maji yazidi mwaika,
Msingi unachimbuka, wazee wameridhika,
Utaifa unatoweka, kwa uchama kuushika,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Babu ameshatoweka, wamebaki vibabuka,
Kwa yao kughafilika, na ya watu kubweteka,
Kaniki zimahamanika, vikoi pia na shuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Waizima Tanganyika, kama sio kunyongeka,
Wahofu ikifufuka, itakuja na mizuka,
Kukumbatia wataka, yao wanaoyataka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Tuteni inafanzika, na mabomu kupigika,
Wao wanayoyataka, kuyafosi kufanzika,
Watuzulia mashaka, kutugharimu viraka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Dunia sasa yataka, madogo ya kushikika,
Makubwa wanaepuka, huwezi kuimarika,
Vivuko hautovuka, mtoni utaanguka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Ushirika wanataka, si'noa iso talaka,
Ukitaka kuachika, pasiwe wa kukuteka,
Hili lisipofanyika, utata hatutaepuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Watu sasa wamechoka, ndani kuwa wawekeka,
Wataka yao kuzuka, hadhi yao kupangika,
Na mambo kunyooka, sio yazidi pindika,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Katiba kama  kibaka, katu haitapendekea,
Ikizua ya kutaka, nani atasalimika ?
Barafu ilogandika, kwanza budi kuyenyuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Barafu ilogandika, kwanza budi kuyenyuka,
Zabzibar wanaotaka, kura huru kupigika,
Kadhalika Tanganyika, Tanzania ikazuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Tatu ndizo tunataka, serikali za hakika,
Ya umoja kuiweka, kcuhangia ushirika,
Ndogo itayojengeka, na watu wenye hakika,
Barafu ilogandika, kwanza budi kuyenyuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Na uchama kupunguka, utaifa kujengeka,
Na kisha ikajazuka, mikoa ya madaraka,
Mfano ukaushika, nchi hii kujengeka,
Barafu ilogandika, kwanza budi kuyenyuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Hili halina mashaka, ajira zitafufuka,
Mikoa ikichemka, ushindani ukazuka,
Uchumi utanyanyuka, na wakazi kuridhika,
Barafu ilogandika, kwanza budi kuyenyuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Mikoa itajengeka, Unguja na Tanganyika,
Na Pemba kuerevuka, ukawaisha wahaka,
Kote nchi kujengeka, kwa ushindani kuzuka,
Barafu ilogandika, kwanza budi kuyenyuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Chama kisichoitaka, hiyo  yetu Tanganyika,
Sio cha Watanganyika, wajua walikotoka,
Sasa kumepambazuka, na ujinga watoweka,
Barafu ilogandika, kwanza budi kuyenyuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Utumwa tulivuka, leo ya nguvu mwataka ?
Weusi mmegeuka, wakoloni wa kuteka ?
Uhuru nusu yafika, nusu nyingine twataka,
Barafu ilogandika, kwanza budi kuyenyuka,
Mafuriko na tufani, ghorofa haina msingi !

Tanganyika, tanganyika

Pacha alishatoweka, mmoja amebakia,
Wapi alipofichika, watu wataka kujua,
Mpotevu asemeka, raia kumfichua,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Tanzania twaitaka, izidi kuendelea,
Pia yetu Tanganyika upya ikazaliwa,
Tuweze yetu kushika, ikawa twajitambua,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Usawa haukufanzika, Tanganyika kuondoa,
Laana ikatufika, mpaka leo balaa,
Yao wanaoyataka, ndio visa wanazua,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Zanzibar na Tanganyika, ndiyo huwa Tanzania,
Mmoja akitoweka, ni kingine kitakuwa,
Msingi hautojengeka, chini utatumbukia,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Hakunao ushirika, upande ukaumia,
Na ubia huponzeka, upande kupendelea,
Ikifika kuhongeka, taabu kubwa inakuwa,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Upofu umetufika, ukweli twaukataa,
Mbali sana itafika, Zanzibar itapaa,
Mamboye ikiachiwa, huru ikajifanzia,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Kadhalika bara pia, miko huru ikiwa,
Waziri mkuu akawa, n dio anaangalia,
Mbali sana itapaa, ngazi ya juu ikawa,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Ni wanasiasa njaa, ukale waliosalia,
Zama wayang'ang'ania, kwa tija yasiyokuwa,
Kwenye juzi wabakia, utandawazi wakataa ?
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Mawaziri watajaa, pamwe na wabunge pia,
Bara na Zzanzibar, na kisha wale wa mkoa,
Ni shule tutajaliwa, viongozi kusomea,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Ushindani utazaa, mazuri yaliyokuwa,
Na watu bora kuibua, mikoani kuwajua,
Taifani kuingia, na ujuzi waliokuwa,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Wakati umefikia, Tanzania kuchagua,
Na kama kuendelea, Tanganyika kurejea,
Mola atatujalia, tuyatakayo yakawa,
Tanganyika, Tanganyika, pacha wake Zanzibar;
hivi nani kamuua ?

Friday, June 1, 2012

D O D O M A

Mji mkuu umekwama, unashindwa kusimama,
Kimejikusuru chama, kubeba Darisalama,
Mshumaa unazima, kufikiria kuhama,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya Ulaya ?

Huko nyuma walisema, katikati na salama,
Nduli aliporindima, kila kitu kikagoma,
Miezi minane ngoma, wakaamba ni lazima,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya DC ?

Miezi minane ngoma, wakaamba ni lazima,
Hata ilipoyoyoma, meli ikazidi zama,
Mzee akanguruma, IMF akaitoma,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya Ulaya ?

Na wajanja wakachuma, uhunzi ulipokoma,
Babu alipotazama, cheche mwisho  akatema,
Kustaafu lazima, nchi  ibaki salama,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya DC ?

Thelathini yatetema, mitatu ingali nyuma,
Toka wapya kuegema, na yao wakayafuma,
Bunge kweli limehama, na chuo kinasimama,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya Ulaya ?

Ila wizara zakwama, nani ataka kuhama,
Mizizi Darisalama, chini imeshajitoma,
Na bahari waipema, upepo mkavu Dodoma,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya DC ?

Sokoine alihama, wao wakarudi nyuma,
Ndwele bado zarindima, zinafichwa ndarahima,
Yapo tusiyoyasema, kuelekea Kigoma,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya Ulaya ?
Wagogo washika tama, haijafika neema,
Ila nyama ya kuchoma, na shingoni zinakwama,
Maji yazidi yoyoma, kuiga Darisalama,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya DC ?
Tabora kwenda lazima, na konani ni Kahama,
Reli yaota mtima, wananchi wanazizima,
Na sasa kwao tuhuma, kuyabeba mataruma,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya Ulaya ?

Nazi kaziye kugema, mnazi ukiufuma,
Kama hauna mtama, na maziwa yasimama,
Bongo zetu ziko nyuma, kuiunda zimekwama ?
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya DC ?

Au suti wazipima, na reli inaroroma ?
Vijana wakijituma, na mtaji wakauchuma,
Kutengeza watakwa, au sisi tunagoma ?
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya Ulaya ?

Uamuzi ni lazima, kitu gani ni Dodoma,
Kuhama au kutohama, sasa wimbo unakwama,
Nchi isiyo azma, kwneda mbele ni gharama,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya DC ?

Miaka inayoyoma, labaki vumbi Dodoma,
Twangonja mwenye huruma, ya kwetu kwnenda yakama ?
Uhandisi wansoma, au vitabu wachoma ?
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au mapya Ulaya ?

Karne hii kiama, kuyafanza tukikwama,
Intaneti kujitoma, vitendo tukavisoma,
Wenyewe tuna lazima, miundombinu kuchuma,
Makao yetu makuu, hivi bado ni Dodoma :
Au ni Dar es Salaam ?