Thursday, June 21, 2012
Mganga hadai mchicha
Mchicha hadai mganga, lakini hudai kuku,
Maombi akiyachonga, si ya mia ni ya buku,
Hata akiwa ni mwanga, ajua hili si huku,
Mganga haagizi tui, aagizacho ni nazi !
Na katu hatojivunga, eti akadai yai,
Ila kama la kuroga, viza lisilostahi,
Kamuone akimwaga, ni maji wala si chai,
Mganga haagizi tui, aagizacho ni nazi !
Mganga haombi kaniki, ila khanga na baibui,
Tena ni ya urafiki, si Mchina hajawahi,
Mengine hashughuliki, kwa kitenge hufurahi,
Mganga haagizi tui, aagizacho ni nazi !
Mganga haombi hela, mizuka watakuomba,
Faraji sio farijala, kama maziwa akiomba,
Haombi kama ya kula, ni ya simba ataomba,
Mganga haagizi tui, aagizacho ni nazi !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment