Juu huvunja sheria, kama chini nao pia,
Ovyo tukiachia, yaja kutugeukia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Sana ukiangalia, udhibiti watakiwa,
Nafasi ikichezewa, tunageuzwa majuha,
Nchi wakaichezea, tukabakia kulia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Kuwabana yatakiwa, baya kutotutendea,
Na kama tukilegea, wenyewe tunaumia,
Nchi huja kuigawa, vitani tukaingia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Madhambi ukichungua, si chini yaanzia,
Huwa kama ni mvua, juu inakotokea,
Ni wapambe haramia, njia humchanganyia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Katika hii dunia, watu wananunuliwa,
Nje wakajinunulia, nchi yao kujakuwa,
Na sisi tulio raia, ikawa twadharauliwa,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Tafakuri asokuwa, tajiri humnunua,
Wao akatumikia, sio nchi kuifaa,
Na hapo mkifikia, udikteta huzua,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Kuwa chini ya sheria, mahakama juu kuwa,
Hofu itawaingia, nafasi wakichukua,
Kuthubutu huhofia, mabaya kutufanzia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Mahakama chini kuwa, nchi ataichezea,
Fujo akatufanyia, kisha kutusingizia,
Haki ikajapotea, matatani kuingia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Jaji mkuu raia, wapaswa kumridhia,
Bunge wakalitumia, yeye likamteua,
Rais huyu ikiwa, huwa zavizwa sheria,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Kuna walionunuliwa, na wao wananunua,
Mfukoni akaitwia, Nyerere katuambia,
Aibu kuwa 'takuwa, nchi kama Tanzania,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Mama yetu ni sheria, na katiba juu yawa,
Kila hali yatakiwa, nyufa zote kuondoa,
Tusije tukajaliwa, kuja rais kichaa,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Ikawa yake sheria, yamlinda kwa udhia,
Dhambi akazizamia, huku twamuangalia,
Amin mnamjua, Uganda yaliyotokea,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Mali akazichukua, na ovyo kujifujia,
Hakuna la kumzuia, tukabaki twazubaa,
Na nyingine kuchukua, Uswizi akazitia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Mke, wana na jamaa, utajiri kuwagea,
Miradi akaiua, ili wao kuwafaa,
Nasi tukayaridhia, kwani hatunayo njia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Usultani kuzua, japo tuliukataa,
Watoto akatamia, cheo chake kuchukua,
Uarabuni twajua, mambo waliyoyazua,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Rais kushtakiwa, lazima kukubaliwa,
Kama akinunuliwa, hataka kumuondoa,
Watu akiwanunua, awe ameshaumia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Wananchi kuwaambia, si chini waliokuwa,
Ila juu wakalia, katiba wakiijua,
Wanaweza kumwondoa, madudu akifanzia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Budi hofu kumtia, nguvu yetu kuijua,
Kazi si kuichezaya. ila ya kuogopewa,
Ovyo tukiachia, midubwana waingia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Zama za kuwasifia, hivi sasa zajisia,
Kazi wamekusudiwa, mzigo kuuchukua,
Tena huru budi kuwa, bila wao kutumiwa,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
Ahadi namuachia, hii ni yake dunia,
Naye analoamua, ndilo hasa linakuwa,
Na wasiojisadia, hawezi wasaidia,
Rais pia raia, wawe chini ya sheria.
No comments:
Post a Comment