Tunzo tunawapatia, kwa sifa zilizopewa,
Hadharani twazitoa, kila mtu kuzijua,
Haki tumeangalia, na zote zahifadhiwa,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo watu kununua, ukubwa kujipatia,
Hamsini ukitoa, huziganga zao njaa,
Vikundi ukinunua, ngazi za juu kupaa,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo jilie nyamaza, yetu kutoyasikia,
Wakubwa tunawatunza, juu waliopitia,
Kisha wakaeneza, kesho yatakayotuua,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo ya ahadi hewa, nayo twawazawadia,
Kwa ahadi kuzitoa, ukweli zisizokuwa,
Tamaa ikabakia, maajabu kutokea,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo nyumba ni anasa, ustwai motokaa,
Na njaa ikitokea, ni chakula kitakuwa,
Karamu kuiandaa, wale raha Tanzania,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo fisadi ni ndugu, hauwezi mkataa,
Hii ni ya kichwa sugu, kinachong'aa kipaa,
Kutunza wetu undugu, kusahau inafaa,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo umaskini dili, misaada kuinyakua,
Wazungu yao akili, burungutu kuachia,
Mtalalia ukili, dhahabu huku watwaa,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo wazungu wa unga, kwa wote wanaojaa,
Wenetu wawachabanga, wao ukwasi wakwaa,
Vidagaa kuwafunga, mapapa huru raia,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo chakula kibovu, pia na hiyo mbolea,
Kwa wale wote werevu, wapatao kwa kutuua,
Mungu awape wangavu, hadi roho kujitoa,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo za kuteuliwa, akili kutoumia,
Sio wa kuchaguliwa, mkoa ukaulilia,
Pasiwe na kidedea, mkoa wahujumiwa,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo ya kubaguliwa, wengine kupendelea,
Hata wasiotufaa, kazi wakaajiriwa,
Maeneo hufulia, yanangoja ogelea,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo fisadi kufaa, wala sio kumuachia,
Huyu mkweli shujaa, atakuja kuwafaa,
Vile tulivyojilia, 'usije jitapikia,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo utumwa sheria, wapewe wanasheria,
Haki wanaojiuzia, dhulluma wakaitia,
Hata wasione haya, kungoja wanachopewa,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo kilimo cha njaa, ni ujanja kutumia,
Mitumba kuinunua, trekta kama bandia,
Mfukoni ukatia, hela inayozidia,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo geuza kibao, haki wanaozinunua,
Kisha wakajiuzia, kwa wakubwa walokuwa,
Tajiri kuwatumia, kama tambaa la mafua,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo rushwa tapakaa, kwa wanaoiachia,
Huku ndani wanalia, ipunguzeni jamaa,
Aibu mnatutia, kila mtu anajua?
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo mikopo hadaa, wapakue na pakua,
Kidogo ukishatoa, kingi ukakichukua,
Nchi yataka kuliwa, ipate kuendelea,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo urongo tumia, wajinga bado wajaa,
Ukweli ukazuia, hakuna watalojua,
Mkono ukishatia, mara moja ni kunawa,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo udhibiti duni, mameneja wachukua
Wasiokuwa makini, vya kwao kuangalia,
Na pengine yumkini, watawala nao pia,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya kutofatilia, wengi hii wamepewa,
Yenyewe yajiendea, Mola anasaidia,
Utabiri kuutoa, vigumu haitakuwa,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo nifae upate, wachache wazawadiwa,
Awali kupanga kete, zinduko kuzinduliwa,
Mwana ni simupopote, huwepo yasiyokuwa,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya mwaga machozi, kuwapa waso hatia,
Akili wasioenzi, kwa nguvu kuzitumia,
Hawanzi mazoezi, mkosa kutambliwa,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo ya maji upupu, mpita njia kumwagiwa,
Na kuachwa utupu, nguo unapozivua,
Ukavitupa vikapu, samaki kujiozea,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya hawa wenetu, wa kwanza kuangalia,
Halafu rafiki zetu, wale kinachobakia,
Asiyekuwa mwenetu, kesho kumfikiria,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo ya mlipa pigwa, kodi yako kutumiwa,
Wewe mwenyewe kupigwa, kwa silaha za kutungua,
Mgalagala kuagwa, fukweni mchanga hujaa,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya maji tope, vijijini kujinywea,
Kisha wazuka mapepe, eti tumeendelea,
Na weusi si weupe, wakoloni weshakuwa,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo ua yafaayo, mfano kujitegemea,
Na michezo kufulia, pasiwe kuendelea,
Wote tunawapatia, hili waliochangia,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya mikopo njaa, watu wetu kuwafaa,
Hii ni ya ujamaa, kama vile kijamaa,
Tundu tunalitumia, cha kwetu kupitishia,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo mifuko ulaji, kuuza na kununua,
Kugawa kwetu mtaji, unene kupindukia,
Wahiji wanaohiji, sisi kazi kupakua,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo za kuwaibia, fukrara wasiojua,
Mifuko kuitumia, ya kwenu nyie kujaa,
Kila mkipungukiwa, ni kisima mwayazoa,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo za simu iba, tafiru wanazotwaa,
Mianya wakaiziba, vyamani ilikojaa,
Mlalahoi kukabwa, kdiogo wakachukua,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya nchi gizani, umeme mtaji kuwa,
Tukiingia nuruni, neema itapotea,
Muhimu kuwa gizani, wafadhili kukamua,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo 'Baah' Ibrahimu, kama kondoo tukawa,
Hata yasiyo na hamu, tukaacha kukosoa,
Twapiga maktaimu, eti mbele twatembea?
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya mweupe bora, hotelini kuwatia,
Na weusi ni hasara, hawajui kutumiwa,
Tena wazidi ukora, na vifo kusingizia,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo ya kula vya umma, kila wakijiuzia,
Wakaziziba tuhuma, na mengine kuhadaa,
Ubepari ni unyama, tumeanza jionea,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunza ya kifaurongo, sauti kuzisikia,
Katiba kupa mgongo, kelele amri ikawa,
Na mwana mlea zongo, haki hana, akapewa,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo mipango sanaa, kipangwacho kutokuwa,
Ikawa waigizia, kama lililotokea,
Watu wabaki wakiwa, dhihaka wanafanziwa,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo udhalililishaji, midude tunagawia,
Wapate la moto taji, zamu yao ikitua,
Karamu ubabaishaji, duniani huishia,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo miradi Ulaji, cha mbele kikitolewa,
Utaifa uhitaji, tumbo linatangulia,
Ambayo sasa wahiji, hata wasio na njaa,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya sahaulisha, madai kutojibiwa,
Watu wakakorofisha, la leo likachelewa,
Ila yao kuyapasha, usiku wakajilia,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo yake potezea, nayo hapa yaingia,
Hoja inapoibuliwa, hewani kaishia,
Bengeni yanaanzia, ikulu ikadandia,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo la wala sinia, kisahani wakatoa,
Matumbo walojaliwa, na akiba kumegewa,
Nundu wanaozilea, kifuani zilojaa,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo chama - baba mama, ukoo na familia,
Tamalaki wajituma, Jetwa wakamfikia,
Kuliokufa hekima, ikabakia udhia,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya kubebeshana, takataka kuchukua,
Kisha ukazilipia, aghali isivyokuwa,
Huku hali wafulia, chakula chakuishia,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo ya njaa wanyama, hifadhini kuwatoa,
Uchumi ukakoroma, yasiyokuwa yakawa,
Wewe ukawa kiyama, cha wanyama Tanzania,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Yuraniamu uhai, tunzo inayotwimbia,
Ienziye maslahi, na ubinafsi kukua,
Hii wote watawahi, uhai wanaotania,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
Tunzo ya dhahabu dili, awamu ya tatu yatwaa,
Walivyojaliwa akili, thamani bue kugawa,
Na mzuka kukabili, mwalimu nao alia,
Tunzo hizi tunawapa, kwa kambi ya washikaji !
Tunzo ya ng'ombe bure, aghali zinazokuwa,
Wamdhihaki Nyerere, na kujifanza wajua,
Na wenye kiherehere, nchi kuja kuiua,
Tunzo hizi tunawapa, wamiliki Tanzania !
No comments:
Post a Comment