Msiwe sawa waumini, moyo uwe akilini,
Elimu mwaithamini, akili zitumieni,
Msibwabwaje kundini, ila palipo yakini,
Viongozi wa kidini, akili 'siwe moyoni!
Sera zenu zinahini, wengi kuwa masikini,
Na fukara ni pagani, au hili hamwamini?
Leeni kwenye imani, kwa kuzifata kanuni,
Viongozi wa kidini, akili 'siwe moyoni!
Msiambe ritadini, kukoma umaskini,
Amani nguo ya ndani, msiikwaze hadharani,
Kwa tendo na ulimini, ufanzeni ulaini,
Viongozi wa kidini, akili 'siwe moyoni!
Rugambwa mkumbukeni, na askofu uchaguni,
Moshi waliyobaini, wakaienzi amani,
Mkiingia kundini, nchi yenda mashakani,
Viongozi wa kidini, akili 'siwe moyoni!
Nyote tunawaenzini, kuwa ni watu makini,
Mwafikia kileleni, shahada mnaauni,
Yaingiyo kichwani, kwa watu yatumieni,
Viongozi wa kidini, akili 'siwe moyoni!
Nyuma katu msibakini, ingineni uongozini,
Sio kwa siasa zaini, ila kwa zenu imani,
Uongozi kubaini, si lazima siasani,
Viongozi wa kidini, akili 'siwe moyoni!
Hapo mlipo mjini, na mkaako vijijini,
Ni viongozi amini, ustawi kubaini,
Watu wote muwapeni, ya hapa hapa duniani,
Viongozi wa kidini, akili 'siwe moyoni!
Isiwe tu ni amani, maendeleo leteni,
Kama mkate amani, na siagi ipakeni,
Hapo ndipo hubaini, ustawi kuauni,
Viongozi wa kidini, akili 'siwe moyoni!
No comments:
Post a Comment