Wednesday, October 31, 2012

Umaskini asili

NITAKUWA ni bahau, tena kweli baradhuli,
Asili nikisahau, yangu na ya Kiswahili,
Babu sasa mjukuu, chabaki kitendawili,
Umaskini asili, katu siwezi 'sahau !

Nende milima na nguu, cha kwangu ni kiswahili,
Ni nusu yake juzuu, bilacho si mtu kamili,
Hujiona ni mafuu, mpungufu wa akili,
Umaskini asili, katu siwezi 'sahau !

Hili ni langu dau, kurudi kwenye asili,
Katu sintokisharau, kwa dhiki na udhalili,
Kama ni kupanda juu, bilacho sistahimili,
Umaskini asili, katu siwezi 'sahau !

Haunifai ukuu, bila asili akili,
Na mali za kijuujuu, mizizi kwao bahili,
Ila lililo mguu, kwenye badi na fasili,
Umaskini asili, katu siwezi 'sahau !

Sio jambo la malau, hii yetu stahili,
Lugha yetu kudharau, ufakiri twakubali,
Vigumu kuenga juu, itakuwa ni muhali,
Umaskini asili, katu siwezi 'sahau !

Ni watu wa chauchau, watufanzia batili,
Wakakataa nafuu, matumzi ya asili,
Wakaifanza juzuu, lugha isiyo awali,
Umaskini asili, katu siwezi 'sahau !

Wanaipiga dafrau, lugha yao ya asili,
Ukubwa wakakubuhu, yetu kufanza dhalili,
Kumbe wanajisahau, zaonyesha zote dalili,
Umaskini asili, katu siwezi 'sahau !

Japani si  mabahau,wajenga kwayo asili,
Na Uchina kwa nahau, sasa ni watu kamili,
Ila tuliojisahau, tusio watu kamili,
Umaskini asili, katu siwezi 'sahau !

Ila tuliojisahau, tusio watu kamili,
Kwa yetu kudharau, washindi ni Waswahili,
Ustawi ni malau, na vimbwanga ndo akili,
Umaskini asili, katu siwezi 'sahau !

No comments: