Mtu mzima akiwa, utoto huukimbia,
Hafanzi la kuambiwa, pasina kufikiria,
Kisha akafuatilia, kila analoambiwa,
Kujibu si kujibu tu, inahitaji akili!
Tafakari huzua, jambo akafikiria,
Na akisha jipimia, mizaniye humwambia,
Lipi la kuliachia, na lipi kung'ang'ania,
Kujibu si kujibu tu, inahitaji busara!
Malau kwenye dunia, kila kona yaelea,
Ukiamua kuvua, itapinduka mashua,
Na wote mlokuwa, ndaniye kuumbuliwa,
Kuibu si kujibu tu, inahitaji hekima!
Hekima tunaiua, sasa kujirpokea,
Hutomjua kichaa, nani mzima akawa,
Wote sasa mnakuwa, dharau mwapalilia,
Kujibu si kujibu tu, inahitaji nadhari!
Chema walichokijua, inakuwa ni sanaa,
Watu wakajichekea, na mizaha kuidhua,
Hadhari ikififia, hatari huzidi kua,
Kujibu si kujibu tu, inahitaji akili!
Kila mjifanya kujua, hili angeling'amua,
Daraja kujipatia, na heshima kuipewa,
Ubabe anayetitia, kiyama atutakia,
Kujibu si kujibu tu, inahitaji busara!
Wa leo Watanzania, haki zao wazijua,
Maguvu mkitumia, hivi kimya watakaa ?
Sasa demokrasia, vingine haitakuwa,
Kuibu si kujibu tu, inahitaji hekima!
Nchi inahujumiwa, watu watayaridhia,
Kauli wasipotumia, ipi iwe yao silaha ?
Mwapaswa kufikiria, kwa hali zao kujua,
Kujibu si kujibu tu, inahitaji nadhari!
Kuandamana ni njia, yaitumia dunia,
Watu wanapozuiwa, bwawa lao litajaa,
La hasira lilokuwa, hadi kingoze kung'oa,
Kujibu si kujibu tu, inahitaji nadhari!
Valvu kifunguliwa, maji huweza pungua,
Tambarae kuingia, salama bwawa likawa,
Vingine haitakuwa, mnatafuta balaa,
Kujibu si kujibu tu, inahitaji nadhari!
Jalali namlilia, kizazi kukiokoa,
Nyota zazusha udhia, giza laanza ingia,
Tuepushe na nazaa, usanii na balaa,
Kujibu si kujibu tu, inahitaji nadhari!
No comments:
Post a Comment