Friday, June 28, 2013

Raia si watoto

Wanalosema wajua, sio wa kutamkiwa,
Watendalo waelewa, sio wa kuelezewa,
Vingine ikitokea, lawama mwajitakia,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Hawajaugua kichaa, na kamwe sio majuha,
Wana lao wakilia, kusikizwa watakiwa,
Vingine inapokuwa, mwaendeleza udhia,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Hata wasiobukua, na elimu kuzivaa,
Majoho kuning'inia, na kupambwa na kofia,
Kichwa tupu walokuwa, haki zao wazijua,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Wafaragua sanaa, na vitendo maridhia,
Visivyoleta ukiwa, na jeraha kuwatia,
Adili ikisinyaa, kimya wategemea?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Hali wanajionea, ghali bure kusifiwa,
Lao wanalolijua, gharama zawalemea,
Hivi waache kulia, sawa mtajionea?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Tofauti zinakua, hakuna la kuzuiwa,
Wa juu waogelea, chini wazama dhiraa,
Sera zimetibuliwa, nani kuwasaidia ?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Kila aliyejaliwa, azidi kuongezewa,
Na yule asiyekuwa, alichonacho mwataa,
Wapi pa kuegemea, ikasikia dunia?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Utundu mwawazuliwa, na ukaidi kuwatia,
Ya kwenu mpate zua, kuezuka na kuezua,
Nani wa kuangalia, ya kwao yaliyokuwa?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Hamaki mnajitia, na vitisho kuvitoa,
Ndimi zinawalemea, madhambi yawachefua,
Nani ni wa kutubia, wakuu au raia?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Vitabu mngefungua, adili mkaijua,
Ukweli mlioua, uanze tena chanua,
Haki mlojizikia, muanze kuzifufua,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Muikomeshe hadaa, na wengine kuonea,
Kwa kuwa mmejaliwa, si wengine kushindiliwa,
Dhuluma huja umbua, haki ikijifungua!
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Kila mwenye kujua, ishara huziagua,
Za wakati zilokuwa, ya kale akaachia,
La, hasha akiendelea, yake huja muumbua,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Ninachowaambia, wakati umewadia,
Mseto kufikiria, mkaepusha balaa,
Imla mkidandia, mtashuka kati ya njia,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Vyote mnang'ang'ania, wenzenu wataridhia?
Kidorik uwaachia, hata kidunchu kikiwa,
Hili msipotambua, uchawi mwaununua,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

No comments: