Sunday, June 2, 2013

Sauti inapozimwa

 Ubabe ukitumika, na haki ikawa nyuma,
Hata wasipolalamika, lao kwa sana huvuma,
Hadi mbali kusikika, na kuongeza tuhuma,
Sauti inapozimwa, kilio chake huzidi!
 
Wingi usiobebeka, hauwezi kunguruma,
Sautiye hukatika, zisifike kwenye ngoma,
Masikio kuzibika, pasiwe kitu kuchuma,
Sauti inapozimwa, kilio chake huzidi!
 
Asiyetaka baraka, hatoipat hekima,
Ya kwake yatafanyika, yakaongeza hasama,
Na mbali hawataruka, balaa kuwaandama,
Sauti inapozimwa, kilio chake huzidi!
 
Ya mola yakikwazika, ya nani kuwa salama ?
Amzuiaye Rabuka, ataka yeye nguruma ?
Au anadanganyika, aipoteze neema ?
Sauti inapozimwa, kilio chake huzidi!
 
Waoga waweweseka, wanaikosa kalima,
Wameshindwa kutamka, wakaondoa dhuluma,
Wanatutia wahaka, kama kweli twenda pema,
Sauti inapozimwa, kilio chake ngurumo!
 
Wingi uliobebeka, kesho isiwe lawama,
Mwenyewe umeyataka, twafumua unafuma,
Kwa shari anayeezeka, akilala huwa wima,
Sauti inapozimwa, kilio chake huzidi!
 
Ninalojua hakika, haki huwa inasema,
KImya kikaondoka, na hoja zake kuvuma,
Kiumbe yote ponzeka, ila si kukosa rehema,
Sauti inapozimwa, kilio chake huzidi!
 
Waasi usiye wahaka, ninaziomba huruma,
Dunia imewateka, hawajui wanazama,
Muqtadiri eleka, utakalo likapema,
Sauti inapozimwa, kilio chake huzidi!

No comments: