Tuesday, February 26, 2013

Mbinuze ni zilezile


Hilo nilitangazile, wa kujua akajua,

Silo linalonogile, mabichwa wakijitia,

Ngoma hii tuchezele, waalikwa twawajua?

Mbinuze ni zilezile, mwele kutibu mganga!


Majini na misukule, huko yalikotokea,

Zumari na vibwagile, mila havijaridhia,

Uliona wapi ndwele, ikaja ikawa dawa?

Mbinuze ni zilezile, ya kichwa kuwa mkia!


Wasemele walewale, kila kitu kujitia,

Wasiokuwa simile, na wakubwa kuwajua,

Wao wakajidhanile, vinara wameachiwa?

Mbinuze ni zilezile, ya juu kuwa ya chini!


Hawakujua upole, ya shujaa tabia,

Na uoga anogile, hadi akadharauliwa,

Na walii si mkwale, neema alijaliwa,

Mbinuze ni zilezile, kushoto kuwa kulia!


Maisha ni kuvukile, madaraja kupitia,

E, mwanangu Chaupele, budi hili kuridhia,

Nalo tulitafutile, halibaki ila dua,

Mbinuze ni zilezile, janibu kuwa ghaibu!


Mchangani liishile, dunia 'kaendelea,

Palepale ubakile, au nawe kufagiwa,

Ina wake wateule, nasi si tunaojua,

Mbinuze ni zilezile, rafiki kuwa adawa!


Waache na kimbelembele, yatakuja kutokea,

Hadharani wapandile, wakicheza kidedea,

Hapo hapo washukile, kwenye vumbi kwogelea,

Mbinuze ni zilezile, halali kuwa batili!


UKifikia kilele, ngwee hautopandia,

Hubakia kushukile, chini kwenda kurudia,

Ukajua lipandile, kushuka ni yake ndia,

Mbinuze ni zilezile, ukweli kuwa hadaa!


Mja hanayo milele, muumbwa kifo kapewa,

Na wakati ufikile, ndiyo ya mwisho hidaya,

Lazima uchukulile, na weye kuchukuliwa,

Mbinuze ni zilezile, mwele kutibu mganga!


Nyie sio wajuvile, haya mambo mwaelewa,

Na wao si waanzile, kitu kuwashtukia,

Zege letu polepole, na haliachi kolea,

Mbinuze ni zilezile, mwele kutibu mganga!


Na lengo ni lile lile, shabaha yenye kujua,

Wateule wenye ndwele, dawa yao kuijua,

Hakika ni wapitile, kuwasindikiza tabia,

Mbinuze ni zilezile, mwele kutibu mganga!


Adili namtanguzile, yanyooka yake njia,

Wala si wa kupindile, na kona kujikatia,

Vya kesho agawalile, mauti visivyojua,

Mbinuze ni zilezile, mwele kutibu mganga!




Atampa mlo gani

 
 
Sijaiona yakini, ninayo shaka moyoni,
Jini kuwa wetu mgeni, sijawa nayo imani,
Naugua ndanindani, wa kumwambia ni nani?
Baba kamleta jini, atampa mlo gani?
 
Ijapo si Selemani, hubaini hadharani,
Namjua huyu nani, na kwenu haonekani,
Naye hajiamini, akinitia machoni,
Baba kamleta jini, atampa mlo gani?
 
Kuna mambo ya uani, hayawekwi barazani,
Huwa huyo afkani, kinyume anayeghani,
Hayawi ya msalani, kuyaleta sebuleni,
Baba kamleta jini, atampa mlo gani?
 
Mshairi mtu gani, kichwani hana maoni,
Ndivyo wanavyoamini, njia wasiobaini,
Kumbe wanajizaini, hatima yao shakani,
Baba kamleta jini, atampa mlo gani?
 
Mtu huyu mtu gani, humuoni kivulini,
Na tonge kwenda kinywani, kwake huwa hayumkini,
Wala kiu haioni, hata akiwa juani,
Baba kamleta jini, atampa mlo gani?
 
Ameniacha pembeni, simo mwake shaurini,
Hakunitaka maoni, wala mie najuani,
Yeye yuko kilingeni, hana asicho baini,
Baba kamleta jini, atampa mlo gani?
 
Kwa heshima ububuni, nimeingia mwandani,
Kofuli iko kinywani, jipya sintolibaini,
Ila nangaoja mwakani, yarudi ya ughaibuni,
Baba kamleta jini, atampa mlo gani?
 
Wengine walibaini, kwa shetani kumuamini,
Watakuwa nayo imani, na dunia kuiwini,
Hivi leo wa shakani, mbele nyuma hawaoni,
Baba kamleta jini, atampa mlo gani?
 
Wamebaki kujilani,  wenyewe kujizaini,
Yakawa kama utani, hawaoni tumaini,
Nchi iko nje ndani, na uchi wajibaini,
Baba kamleta jini, atampa mlo gani?
 

Monday, February 18, 2013

BARAZA LA KISWAHILI TANZANIA

 
KIZIBAO kimekua, baraza ilivyokuwa,
Wizara limekivaa, au limeshavuliwa,
Lugha yatima ikawa, hakuna kuendelea,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Linazidi kudumaa, na wakati unapaa,
Mengi lingeyaamua, kama huru lingekuwa,
Miradi likaizua, trilioni kuingia,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Kawaida imekua, kaaburini limetiwa,
Nani alikumbukia, au hazina kujua,
Tukilichangamkia, mengi laweza kuzaa,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Tumejenga mazoea, kukazwa nazo sheria,
Ndimo tunamoishia, hatutaki kujitoa,
Watazuka wakujua, lugha mtaji ikawa,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
Mtaji twauachia, ujasiriamali kuvia,
Kwa elimu na sanaa, nchi vingelichangia,
Hata kibiashara pia, masoko yangesambaa,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Tipu tipu alijua, biashara kaanzia,
Tanganyika ikakua, hadi Kongo kuingia,
Leo ninayojionea, nje tunakuhofia,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Tunabaki kurejea, ndani tuking'ang'ania,
Mwee zabanana kuwa, si moja moja kumea,
Jopo hatujajaliwa, uchumi kufikiria,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Laiti ningelikuwa, kuna mengi ya kuzua,
Redio zinalilia, na tivii nazo pia,
Ila ninayosikia, uwezo wanafulia,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Uwezo ningelipewa, ngwee ningejikatia,
Kwa kuenzi teknolojia, na programu kuzua,
Vijana wakatulia, na vichwa kuvifungua,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Uzuzi ungelikuwa, ujasiriamali kwenea,
Kwa maabara kuanzia, ya lugha za Tanzania,
Makao makuu ya mkoa, mradi ungeanzia,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Wadau ningewambia, lugha tumeipania,
Kila njia kutumia, na vyuoni kuingia,
Na kituo cha kwanzia, cha Baraza kingekuwa,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Nimeishawaelezea, hapa ninamalizia,
Akili tukitumia, tupate la kuamua,
Lugha isipotumiwa, kwoza haitachelewa,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!
 
Manani twakulilia, lugha yetu kujalia,
Tupate kuitumia, kwa imani na dunia,
Juu tukajipandia, na kilele kufikia,
Baraza la Kiswahili, bora liwe mamlaka!

HATIMA YA KISWAHILI


LUGHA hii ni azizi, yenye kubwa manufaa,

Laiti tungemaizi, hazina tungetumia,

Ila wetu uongozi, Ukingali wasinzia,

Hasara ya Kiswahili, kaida ni kiada hakuna.

 

Tipu tipu kamaizi, Kongo akenda kutua,

Biashara kwa kuenzi, Tanganyika ikapaa,

Tukayafanya majenzi,leo tunayochelea,

Hasara ya Kiswahili, Tipu tipu katushinda!

 

Nyumbani na pande hizi, lugha wangeitumia,

Kuuza na manunuzi, mabishano kuingia,

Vipya vizuke kwa jozi, hadi ziada ikawa,

Hasara ya Kiswahili, jirani kutozungumza.

 

MS watuenzi, lugha wameiandaa,

Iko katika ngamuzi, kama hujasimuliwa,

Ukiwa na vitowezi, waweza soma dunia,

Hasara ya Kiswahili, tovuti zetu zinapwaya.

 

Ukafanza mamkuzi, na hali  watu kujua,

Kunavyo vipeperuzi, waweza kuwarushia,

Dunia sasa pembuzi, ni kijiji imekuwa,

Hasara ya Kiswahili, unyani unatuzidi.

 

Twakosa maandalizi, nje kwenda palilia,

Yanazidi maongezi, vitendo vimepungua,

Bado iko kubwa kazi, ujasiriamali ikawa,

Hasara ya Kiswahili, kutotawala Afrika.

 

Wanangoja uwekezi, hili washindwa tambua,

Yakifanzwa ma'ndalizi, bilioni kuingia,

Kwa elimu nazo kazi, nchi kutokufulia,

Hasara ya Kiswahili, kaida ni kiada hakuna.

 

Kiingereza chenye enzi, sasa chaachia njia,

Dunia sio mjenzi, moja tu kuitumia,

Inataka mapinduzi, ndani na nje kutiwa,

Hasara ya Kiswahili, Tipu tipu katushinda!

 

Inataka mageuzi, asili kuichungua,

Pakawepo kikomezi, mazoea kuachia,

Ili tuipande ngazi, kule tunakotakiwa,

Hasara ya Kiswahili, jirani kutozungumza.

 

Lugha yataka malezi, na uwekezi kutiwa,

Kukusanya wajuuzi, mifumo kuifumua,

Tukifanza mapinduzi, vyungu viwe vimejaa,

Hasara ya Kiswahili, tovuti zetu zinapwaya.

 

Tafsiri sio kazi, vikundi tukichangia,

Masomo yote asisi, tunaweza kutohoa,

Istilahi kimakuzi, mlima mkubwa ukawa,

Hasara ya Kiswahili, unyani unatuzidi.

 

Kwa kutumia ngamizi, vitu vyote vikatiwa,

Wakaanza mazoezi, wana shule kusomea,

Wanapopata tatizi, ufumbuzi kupatiwa,

Hasara ya Kiswahili, kutotawala Afrika.

 

Tukiyafanya malezi,  kompyuta kutumia,

Lugha yetu tukaenzi, sana mbali kufikia,

Wenetu wana uzuzi, mengi watayagundua,

Hasara ya Kiswahili, kutotawala Afrika.

 

Jitihada hatufanzi, kompyuta kuwekewa,

Wakaanza mazoezi, hadi wakazizoea,

Kisha kwenye utumizi, mapya wakayavumbua,

Hasara ya Kiswahili, kutotawala Afrika.

 

Ukifanya uchunguzi, tofauti utajua,

Wasio na mazoezi, vijijini wamejaa,

Wao kwanza utambuzi, tivii huidhania,

Hasara ya Kiswahili, kutotawala Afrika.

 

Wa mjini wenye wenzi, zana wakawapatia,

Wayaweza matumizi, kila aina wajua,

Kuwatega huwa kazi, wao watakuchezea,

Hasara ya Kiswahili, kutotawala Afrika.

 

Tungeiacha ajizi, kompyuta kuenea,

Ili lugha kuienzi, Kiswahili kikakua,

MS ni wajuzi, hima watatufanzia,

Hasara ya Kiswahili, kutotawala Afrika.

 

Ninamuomba Mwenyezi, macho  akatufungua,

Tukaulola na mwezi, kule unakoishia,

Ya kale tukiyaenzi, kama nyani twabakia,

Hasara ya Kiswahili, kutotawala Afrika.

 

Uswahili kitu gani?

 
Mswahili, mswahili, atumia Kiswahili,
Lugha yake ya asili, kwalo hilo si bahili,
Ajivuna kwa halali, si haramu kunakili,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!
 
Wala sio udhalili, au kukosa akili,
Hiyo dhana baradhuli, watoa dhoofu hali,
Waliokosa akili, kwa utumwa kuwa mali,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!
 
Ni yangu ardhilhali, iwafikie bilkuli,
Neno hili kulhali, zama zake zawasili,
Umma umeshakubali, vizuizi ni makuli,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!
 
Katiba itafasili, na kukipandisha hali,
Vya wengine si batili, ila nafsi ya pili,
Hili lisipowasili, kuendelea muhali,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!
 
Nilsema ni muhali, watumwa kustahili,
Historia kuwajali, kwa kutnza kiswahili,
Zama zao zimefeli, jalalani zao feli,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!
 
Heshima ya Uswahili, kupata mzawa asili,
Lugha aisyekejeli, heshima kuwa wakili,
Cheo akikidahili, likawa hilo halali,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!
 
Nishani kustahili, dunia kumsabili,
Halihitaji akili, linataka uhalali,
Zama hizi Kiswahili, cheo kinastahili,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!
 
Iwe Mchina mithili, ukiitwa Mswahili,
Na uzazi ni wa mbali, si nchi kustahili,
Watatoka Rwanda kweli, na waitwe Waswahili,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!
 
Lugha atakayejali, ndiye awe Mswahili,
Astahili medali, japo kwao si asili,
Kina wetu bure ghali, waishie udhalili,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!
 
Ninakuomba Jalali, tuongoze Waswahili,
Kwa lugha tuwe kamili, hadi kwenye  uzamili,
Kitumike Kiswahili, kwa akheri na awali,
Uswahili ni asili, lugha na utamaduni!