Monday, October 14, 2013
KIKULACHO
Kwanza 'ngejiangalia, vizuri kujichungua,
Wa nje kutosingizia, masahibu wakutia,
Pengine hujatambua, ndaniyo aweka kuwa,
Kikulacho uko nacho, unacho nguoni mwako!
Labda keshakuingia, kwa mithili yake chawa,
Kwenye nywele kaingia, pango keshalilipia,
Anasa ajifanzia, rusha roho azizua,
Kikulacho uko nacho, unacho nguoni mwako!
Stihizai hutia, wengine ukadhania,
Shere akautezea, jirani kusingizia,
Ila yatakustua, kung'atwa ukigundua,
Kikulacho uko nacho, unacho nguoni mwako!
Damu anajinyonyea, kuwanda akazidia,
Wewe unapalilia, yeye anajivunia,
Au ng'ombe umekuwa, kaziye kukukamua,
Kikulacho uko nacho, unacho nguoni mwako!
Yako unaharibikiwa, yake yanasimuliwa,
Kichinichini ikawa, kitu hautosikia,
Husema amepatia, mahala kashikilia,
Kikulacho uko nacho, unacho nguoni mwako!
Utamu kashikilia, hawezi kupungukiwa,
Ila niavyotambua, kuna siku yaingia,
Nywele ukijakunyoa, atakosa pa kukaa,
Kikulacho uko nacho, unacho nguoni mwako!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment