Monday, October 14, 2013
USIMSOGELEE
HATA dadayo akiwa, simsogelee mnafiki,
Stara hajajaliwa, rohoye ni mamluki,
Ndarahima adhania, Mola wake wadhihaki,
'Simsogelee mnafiki, mwisho atakuumbua !
Kiumbe ninakataa, hajawa naye rafiki,
Kazi yake kfukua, udhaifu kuulaki,
Kisha akakufanzia, ya kuja kutaharuki,
'Simsogelee mnafiki, mwisho atakuumbua !
Kifo atakuombea, ami wa kindakindaki,
Huku anakutekea, nawe wampa malaki,
Au unalomfaa, pasina nayo mikki,
'Simsogelee mnafiki, mwisho atakuumbua !
Dhiki atakuombea, njiani ije kulaki,
Kadri unavyofulia, furaha haimtoki,
Yake yakiogelea, kuzama yako huafiki,
'Simsogelee mnafiki, mwisho atakuumbua !
Usoni hukuchekea, hali moyoni ni chuki,
Hutaka kumalizia, ya uimbeya kuafiki,
Kisasi akakitia, msingi kisichonaki,
'Simsogelee mnafiki, mwisho atakuumbua !
Pagani ninakwambia, bora yake mnafiki,
Kisomo hajakijua, nafsi ingeafiki,
Dua ukimuombea, hudumu kwa urafiki,
'Simsogelee mnafiki, mwisho atakuumbua !
Dini hukurubia, mwisho akaiafiki,
Ashaduu akatia, akapendezwa Mulki,
Ila ninalikataa, hayawezi mnafiki,
'Simsogelee mnafiki, mwisho atakuumbua !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment