Monday, October 14, 2013
MNAPOKUWA SHULENI, VYUONI
WENGI nimeuliziwa, waliokuwa vipenzi,
Rafiki wa kutulia, tusofendana ajizi,
Habari nikaambiwa, dongo halikuwaenzi,
Mnapokuwa shuleni, hebu ishini kwa wema:
mwaweza msionane, tena baada ya hapo!
Najua wa chekekechea, wamerdi kwa Mwenyezi,
Jichoni sikuwatia, nilipoianza kazi,
Taarifa sikupewa, si za jana si za juzi,
Mnapokuwa shuleni, hebu ishini kwa wema:
mwaweza msionane, tena baada ya hapo!
Msingi na huko pia, tumepishana kwa ngazi,
Peter alishapotea, na Ummy naye ni wa juzi,
Sasa ninasimuliwa, na hata wangu wanafunzi,
Mnapokuwa shuleni, hebu ishini kwa wema:
mwaweza msionane, tena baada ya hapo!
Sekondari tulijaa, pasina ya kizuizi,
Milango tulotumia, ya shule ile Mawenzi,
Wameondoka mamia, na kujua si wajuzi,
Mnapokuwa shuleni, hebu ishini kwa wema:
mwaweza msionane, tena baada ya hapo!
Chuo kikuu najua, kwa hesabu siiwezi,
Waliojiondokea, kina kazi kikotezi,
Sammy analialia, ya Freddy, Mboya vipenzi,
Mnapokuwa shuleni, hebu ishini kwa wema:
mwaweza msionane, tena baada ya hapo!
Rafiki aliyekuwa, na pili ni mkufunzi,
Dunia yatuhadaa, ila yake hatuwezi,
Lati tungelijua, mambo yepi ya kuenzi ?
Mnapokuwa shuleni, hebu ishini kwa wema:
mwaweza msionane, tena baada ya hapo!
Ukaribu tusokuwa, tumuachia Mwenyezi,
Siri zake azijua, mapenzi hatuyawezi,
Huenda kwa kuandikiwa, zikabaki simulizi,
Mnapokuwa shuleni, hebu ishini kwa wema:
mwaweza msionane, tena baada ya hapo!
Mola namwangukia, aliye wetu mlinzi,
Hao walotangulia, kuwapa njema hifadhi,
Viwango anavijua, hilo kwangu mwanafunzi,
Mnapokuwa shuleni, hebu ishini kwa wema:
mwaweza msionane, tena baada ya hapo!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment