Monday, October 14, 2013

UKIZIDISHA UCHOYO


Angalia historia, toka utoto wakiwa,
Shuleni tulipokuwa, dishi walilivamia,
Kingi wakajimegea, kidunchu kikabakia,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

Chuoni tumeingia, sasa ninakumbukia,
Shimoni kulimokuwa, chakula tukigombea,
Mara mbili warejea, ngwini tulipokaangiwa,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

Yaendelea tabia, ukubwani kuingia,
Nchi wanajimegea, wengine kutogeea,
Nafsi yawachezea, kumg'ang'ania dunia,,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

Ila ninayahofia, walivyochoka raia,
Furaha yawakimbia, na hasira kuwajaa,
Kulipuka ndio njia, nalilia Tanzania,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

Tuidhibiti tabia, yenye wingi wa tamaa,
Ovyo kujilimbikia, hata kwa yasiyotufaa,
Yataja tutumbukia, tukabaki tunalia,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

Mmoja tungeanzia, mitaani kuingia,
Makubwa hayajakuwa, matatizo Tanzania,
Madogo yanayokuwa, tusiache kutatua,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

Upofu tukijitia, twampa shoka kichaa,
Wana na wanaofatia, salama hawatakuwa,
Mbegu tutajipandia, ya hasama na adawa,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

Uchoyo ukizidia, kupendwa haitakuwa,
Watu watakuchukiya, na unafiki kutia,
Ilhali wazomewa, udhani washangiliwa,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

Rafiki watakimbia, mwenyewe ukabakia,
Ikawa wao umbeya,  tadi kuiongelea,
Mengi wakakupakia, weye usiyechukua,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

Kama kuna majaliwa,  hili nisingejaliwa,
Riziki ningeachia, kila mtu kujaliwa,
Yangu nikawagawia, tunu kwenda zawadiwa,
Ukishazidi uchoyo, wengi watakuchukia !

No comments: