Monday, October 14, 2013

P U L I Z O

Upepo ukilitia, kwa kiasi hufumuka,
Hupanuka likajaa, na viungo kuitika,
Usipolishikilia, juu laweza chomoka,
Pulizo likishajaa, mwisho wake kupasuka !

Arijojo hukimbia, kwenda lisikokutaka,
Wahaka ukakujaa, hali unaweweseka,
Huwezi likimbilia, si kiumbe wa kupaa,
Pulizo likishajaa, mwisho wake kupasuka !

Jua litaliachia, hali mahala kufika,
Hari ikishazidia, kawaida kufumuka,
Na viumbe wanajua, jambo hili la hakika,
Pulizo likishajaa, mwisho wake kupasuka !

Hawataki kusikia, ukawatia mashaka,
Ya kwao yakasinyaa, waendako kutofika,
Wanaipenda hadaa, kwa kuzua na kuzuka,
Pulizo likishajaa, mwisho wake kupasuka !

Juu wanaidhania, furaha imefichika,
Nini utawaambia, wasiache kuteseka,
Ukichaa inakuwa, eti ni shani kuzuka,
Pulizo likishajaa, mwisho wake kupasuka !

Mbio wanazitimua, haraka wapate fika,
Ushindani kuutia, hata pasipotakika,
Malaika wavizia, nani wataoanguka,
Pulizo likishajaa, mwisho wake kupasuka !

Kamba wameshazitia, na viuzi kuviweka,
Kuruka asiyejua, huenda akateguka,
Pumzi wanaoishiwa, hao mabli kutofika,
Pulizo likishajaa, mwisho wake kupasuka !

Hii halina ngekewa, kadara yahitajika,
Kila asiyeijua, haiwezi nunulika,
Bure unajisumbua, akiba ungeiweka,
Pulizo likishajaa, mwisho wake kupasuka !

Kalamu naiachia, hapa ninapumizka,
Siwezi ya kukimbia, kutembea natosheka,
Umri nikiongezewa, ukweli kudhihirika,
Pulizo likishajaa, mwisho wake kupasuka !

No comments: