Thursday, December 13, 2012

T H A W A B U

Thawabu utagawiwa, mema ukijifanyia,
Watu ukasaidia, kwa huruma kuwalea,
Bali bado sijajua, dhambi haitonizidia,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Ya nje tunayajua, ya ndani twakadiria,
Milima ukipangua, mabonde yatabakia ?
Safari naihofia, hatari nyingi zajaa,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Umbali nashuhudia, kamili sijaujua,
Na siku ya kufikia, ni hadithi imekuwa,
Mitihani imejaa, kufaulu ninagwaya,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Mitego imesambaa, unaweza kushitua,
Vipini kukuingia, na miiba usiyotoa,
Miguu ikalemaa, mbele usende tembea,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Dharau naihofia, yaweza kuniingia,
Thawabu zikatwaliwa, na mwingine kwenda pewa,
Udhaifu nikijua, waweza kuniokoa,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Wahaka waniingia, ujibari kutokea,
Utukufu nikavaa, kwa joho la kushonewa,
Na rangi nikapambiwa, kiumbe kwenye dunia,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Uovu nauhofia, usije kuniingia,
Ubaya kukusudia, kwa kisasi kujitia,
Milima hukwanguliwa, vichuguu kubakia,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Hofu inaniingia, kila  ninapowazia,
Shetani kunihadaa, rafiki nikamdhania,
Kwaye kuniongopea, mkenge nikaingia,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Kilio chako chamkera

Mgumu kuvumilia, na subira humpaa,
Kilio ukiangua, huku unaugulia,
Atauona udhia, hataki kukisikia,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Mgonjwa ukitambua, ni mgumu kujijua,
Yeye anaugulia, sio mbwembwe anatia,
Wewe ukimatania, ndugu yangu wakosea,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Waweza kumdhania, ni sanaa anatia,
Uchungu yeye ajua, vipi wewe kuujua,
Hali ungelijaliwa, hapo usingelikaa,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Mwenye njaa hugugumia, mwenye shibe kafakamia,
Vipi atamuelewa, mkosa asojaliwa,
Tumbo humngurumia, kama ndege ya Ulaya,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Chakula ajionea, ashindwa kukinunua,
Kabaki kukiangalia, kwake sasa ni sanaa,
Wamsimanga raia, mikono atanyanyua,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Palikuwa Malkia, Ufaransa nasikia,
Watu wakamwendea, mikate wanalilia,
Yeye akawashangaa, keki kutokununua,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Shilingi asiyekuwa, vipi maji 'tanunua,
Kiu humashambulia, akatamani kulia,
Mengine ukimwambia, vipi atakuelewa?
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Hatuishi kuzubaa, wnezetu kuporomoa,
Majumba yazidi ng'aa, na shani za motokaa,
Ila mfukoni balaa, senti zinatukimbia,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Haruna Kilewo mbia, zamani aliyekuwa,
Kilio akiangua, hivi sasa kafulia,
Auni aililia, wapi  pa kuingilia,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Mola tunawaombea, mliokuwa mughni,
Mkijatufikiria, tutapata afueni,
Mioyo ikatulia, tudhani tuna thamani,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Kilio chako chamkera

Mgumu kuvumilia, na subira humpaa,
Kilio ukiangua, huku unaugulia,
Atauona udhia, hataki kukisikia,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Mgonjwa ukitambua, ni mgumu kujijua,
Yeye anaugulia, sio mbwembwe anatia,
Wewe ukimatania, ndugu yangu wakosea,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Waweza kumdhania, ni sanaa anatia,
Uchungu yeye ajua, vipi wewe kuujua,
Hali ungelijaliwa, hapo usingelikaa,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Mwenye njaa hugugumia, mwenye shibe kafakamia,
Vipi atamuelewa, mkosa asojaliwa,
Tumbo humngurumia, kama ndege ya Ulaya,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Chakula ajionea, ashindwa kukinunua,
Kabaki kukiangalia, kwake sasa ni sanaa,
Wamsimanga raia, mikono atanyanyua,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Palikuwa Malkia, Ufaransa nasikia,
Watu wakamwendea, mikate wanalilia,
Yeye akawashangaa, keki kutokununua,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Shilingi asiyekuwa, vipi maji 'tanunua,
Kiu humashambulia, akatamani kulia,
Mengine ukimwambia, vipi atakuelewa?
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Hatuishi kuzubaa, wnezetu kuporomoa,
Majumba yazidi ng'aa, na shani za motokaa,
Ila mfukoni balaa, senti zinatukimbia,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Haruna Kilewo mbia, zamani aliyekuwa,
Kilio akiangua, hivi sasa kafulia,
Auni aililia, wapi  pa kuingilia,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Mola tunawaombea, mliokuwa mughni,
Mkijatufikiria, tutapata afueni,
Mioyo ikatulia, tudhani tuna thamani,
Kukerwa yake tabia, 'gonjwa asiyelijua !

Thursday, November 29, 2012

Vijiji sio Ulaya

KUZURU mapambo huwa, kitu kisichosadia,
Ni mkubwa udhia, wanavijiji wajua,
Wao mbuga hawajawa, wanyema kuangalia,
Vijiji sio Ulaya, mnaenda kutembea ?

Nchi kuendelea, makada wanatakiwa,
Vijijini kwenda kaa, mema wakayaamua,
Dhiki wakizielewa, ni rahisi kutatua,
Vijiji sio Ulaya, mnaenda kutembea ?

Ukenda kutembelea, nini utakiongea,
Watu hukuangalia, mate wakajitemea,
Shere mnawachezea, wala dawa  hamjawa,
Vijiji sio Ulaya, mnaenda kutembea ?

Kwingine watachimbua, afu wakajipatia,
Hawatakutegemea, mjini unaykeaa,
Mzigo umeshakua, kiondoka huridhia,
Vijiji sio Ulaya, mnaenda kutembea ?

Kijijini ukikaa, mengi utayasikia,
Tena ukajionea, mepesi yaliyokuwa,
Ila miamba yakaa, ugumu wakautia,
Vijiji sio Ulaya, mnaenda kutembea ?

Vijisenti kadhaa, matatizo hutatua,
Watu wakachekelea, na dua kukuomboa,
Mpango ukiuzua, bora hujayakazaliwa,
Vijiji sio Ulaya, mnaenda kutembea ?

Akili mkitumia, vijijini mtakaa,
Babu tunamtambua, hawa aliyojaliwa,
Butiama alikaa, tena akijilimia,
Vijiji sio Ulaya, mnaenda kutembea ?

Ardhi budi kujua, kitovu yakichukua,
Nayo si ya kuiachia, watakiwa kurejea,
Kwa muda ukendakaa, kiungo kinarejea,
Vijiji sio Ulaya, mnaenda kutembea ?

Akili huzifungua, ukaanza pambanua,
Ya jua na ya mvua, tofauti ukajua,
Na kisha ukiamua, manufaa huzaliwa,
Vijiji sio Ulaya, mnaenda kutembea ?


Saturday, November 10, 2012

Njaa inapotawala


Watu wanapoumia, kwayo kiu nayo njaa,
Huku jua lapaua, kichwani kilichokuwa,
Kisha wazidi udhia, wema kutojionea,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Nchi wanapopakua, kama yao vile kuwa,
Vitamu wakajilia, na akibani kutia,
Huruma ikapotea, roho mbaya ikakua,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Cha wengi  kinapoliwa, mmoja kujishibia,
Haya ikendaugua, na 'spitali kutibiwa,
Na aibu  kulemaa, ukabakia ukiwa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Maji yanapopotea, dhahabu nayo yakawa,
Watu wakajisifia, ya msingi kujaliwa,
Kicheko wakaangua, raia wakifulia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Maji wanapokataa, muhimu hayajakuwa,
Hesabu yakatungiwa, kasoro yaliyokuwa,
Kifanzwacho kisokuwa, zikaingia sanaa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Giza wa kijivunia, na nuru kuikataa,
Kwa hadaa  kuzidiwa, kiatu kugeuziwa,
Huwashangaa dunia, mgongo kuwaachia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Elimu ikivuliwa,  nguo iliyoivaa,
Matambara ikapewa, na bomba za kuchakaa,
Maji zisizoyatoa, ila kelele na hewa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Mengi huyafikiria, ya ufakiri na njaa,
Sahaba kuwafukua, na hekima ilokuwa,
Ukweli nikaujua, yao na Islamiya,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Wao ndio watwabia, kilimo kwanza ni dawa,
Kumbe njia watumia, kinyume zilizokuwa,
Na sasa twajionea, shere yanatuchezea,

Heri fakiri ukawa, wa mali kwenye dunia,
Lulu waweza ivua, mara tajiri ukawa,
Dunia ikakujua, nawe uliipitia,

Heri fakiri ukawa, wa elimu kutokuwa,
Wengine watakufaa,za kwako ukajitia,
Nawe ukatumia, uweze kujichumia,

Ila ni kubwa balaa, fakiri wewe ukiwa,
Uongozi kuishiwa, ufakiri ukavaa,
Haitokufaa daawa, kila kitu hufulia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Hufulia ya kufaa, iwe jalala na jaa,
Dhahabu ukiipewa, chini utaichimbia,
Au bahati ikiwa, bure wewe utagawa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !
Fakiri wa kuongoa, ndio mama wake njaa,
Nchi yote huishiwa, ombaomba kubakiwa,
Hata wakajisifia, uongo unabakia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Uongo ukazaliwa, kwa uongozi wa njaa,
Watu wakapakuliwa, maneno yaliyoyaa,
Kitu yasiyokujakuwa, ila kuongeza makiwa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Hudai kuendelea, na watu walala njaa,
Takwimu hutapikiwa, zinazonuka hadaa,
Hali ukiangalia, ubaki jisikitikia,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Vipimo  hujiokotea, dampo vilivyotupiwa,
Hadharani kutumia, aibu vilivyojaa,
Watu wakakebehiwa, na ukweli wasojua,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

Njaa mama wa balaa, mlango twamfungulia,
Na huku twajiendea, kama kitu haijawa,
Lusifa afurahia, mavuno mengi yakawa,
Njaa inapotawala, huwa mtihani mkubwa !

WAKOMA MWABAKI NAO ?

 TABIA akigundua, kuonya kaamriwa,
Mwapasa kuyasikia, kutengwa budi ikawa,
Kati mkiwaachia, wengine wataugua,
Wakoma  huwa watengwa, kuyaepuka madhara !

Rushwa tumeitambua, ni ukoma waingia,
Kimya tukijikalia, itakuja tuumbua,
Umma naushadidia,  hili kuja lihofia,
Wakoma huwa watengwa, kuiepuka hasara !

Kut9jua nakataa, hilo haliwezi kuwa,
Huruma tumeingia, utadhani ni ukiwa,
Macho tunalifumbia, liletalo kulemaa?
Wakoma  huwa watengwa, kuyaepuka madhara !

Tunatia ujamaa, na udugu kutetea,
Karibu tunawajua, pembeni hawajakaa,
Tutumialo sinia, hilohilo watumia,
Wakoma huwa watengwa, kuiepuka hasara !

Lawama tukizitoa, nini zinasaidia,
Au aibu na  haya, huwa hapo zapotea,
Na katika  jumuiya, ndo pekee walokuwa ?
Wakoma  huwa watengwa, kuyaepuka madhara !

Kuna mengine udhia, mtu ukifikiria,
Mafuu utadhania, jinsi tunavyoamua,
Au kama twachezewa, kutogwa na wasiokuwa,
Wakoma huwa watengwa, kuiepuka hasara !

Mizizi tunaing'oa, kwa majani twapandia ?
Mbuyu haijakuwa, watu kuja kushangaa,
Watauona mzaha, wakacheka na kulia,
Wakoma  huwa watengwa, kuyaepuka madhara !

Ujumbe umetimia, imebaki kuamua,
Salama kutopotea, Tanzania wangojea,
Maamuzi kusikia, ulua yaliyojaa,
Wakoma huwa watengwa, kuiepuka hasara !

Treni bila dereva

 Muongoza bila kuwa, garimoshi hupwelea,
Watu likawatishia, nje, ndani walokuwa,
Usalama hupotea, maafa mkahofia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Na ndani unapokaa, budi kutazama njia,
 Wapi mnaelekea, na kama salama yawa,
Vingine inapokuwa, breki ukazitia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Treni bila dereva, lazima kuacha njia !
Kona ukazitambua, na harari zilokuwa,
Ovyoovyo kijiendea, watu utaparamia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Vilima usipojua,na mteremko ya njia,
Huangusha mabehewa, kilio kikubwa kuwa,
Vyuma vikajichimbia, na vingi kujipindia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Dereva anatakiwa, chombo kukihudumia,
Njiani kujipitia, wote salama wakawa,
Vingine inapokuwa, uhai twauchezea,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Wapo wakudandia, na rafiki walokuwa,
Usije kuwaachia, bure wakajipandia,
Au za hongo wakanunua, tiketi zio bandia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Hasara utaingia, shirika kuja jifia,
Kitambo ukiridhia, milele hudidimia,
Dunia hutuchezea, mitihani tulopewa,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Mawasiliano kivia, vingine hautajua,
Nyingine weza ingia, kwa mambo ya kusikia,
Hatari kubwa ikawa,kwa maisha na rupia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Dereva atarajiwa, kazi moja kuifaa,
Nyingine akichukua, anaweza kuzidiwa,
Kija kutahamakia, mkenge mmeingia,
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !

Safari yaashiria, dereva hatujamjua,
Na treni yakimbia, breki haijatiwa,
Sisi tunaposhangaa, wengine wachekelea ?
Treni bila dereva, lazima kuacha njia !