Thursday, December 13, 2012

T H A W A B U

Thawabu utagawiwa, mema ukijifanyia,
Watu ukasaidia, kwa huruma kuwalea,
Bali bado sijajua, dhambi haitonizidia,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Ya nje tunayajua, ya ndani twakadiria,
Milima ukipangua, mabonde yatabakia ?
Safari naihofia, hatari nyingi zajaa,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Umbali nashuhudia, kamili sijaujua,
Na siku ya kufikia, ni hadithi imekuwa,
Mitihani imejaa, kufaulu ninagwaya,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Mitego imesambaa, unaweza kushitua,
Vipini kukuingia, na miiba usiyotoa,
Miguu ikalemaa, mbele usende tembea,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Dharau naihofia, yaweza kuniingia,
Thawabu zikatwaliwa, na mwingine kwenda pewa,
Udhaifu nikijua, waweza kuniokoa,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Wahaka waniingia, ujibari kutokea,
Utukufu nikavaa, kwa joho la kushonewa,
Na rangi nikapambiwa, kiumbe kwenye dunia,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Uovu nauhofia, usije kuniingia,
Ubaya kukusudia, kwa kisasi kujitia,
Milima hukwanguliwa, vichuguu kubakia,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

Hofu inaniingia, kila  ninapowazia,
Shetani kunihadaa, rafiki nikamdhania,
Kwaye kuniongopea, mkenge nikaingia,
Thawabu utazipata, je, zitazidi madhambi ?

No comments: