Thursday, May 30, 2013

Kila mkweza ukubwa



Ukimuona raia, debe anajipigia,

Mkubwa kumnyanyua, hadi awe nazo mbawa,

Huyo ukimchungua, siriye utaijua,

Kila mkweza ukubwa, na yeye autamani!

 

Yazusha yetu dunia, mitume wa kuamua,

Cheo wakajitwalia, na karama kununua,

Kisha wakaja chipua, mithili yake maua,

Kila mkweza ukubwa, na yeye autamani!

 

Huyo ukimuangalia, ukubwa aulilia,

Na njiaye ya kupitia,  mkubwa kwanza kupewa,

Kisha aje kufatia, apewe alichopewa,

Kila mkweza ukubwa, na yeye autamani!

 

Hawa watu wa tamaa, waidanganya dunia,

Ndivyo wanavyofikiria, kumbe la hasha waugua,

Yumkini ukichaa, tena wa kuchanganyikiwa,

Kila mkweza ukubwa, na yeye autamani!

 

Waishi kwa kupagawa, na ushindani kuzua,

Wa ovyo ulokuwa, kufuru unaotia,

Hakika nawaambia, washindwe na kulegea,

Kila mkweza ukubwa, na yeye autamani!

 

Fakiri wetu walia, makubwa twende vamia,

Gari ukijitolea, mafutaye pia lipia,

Tana karne ikiwa, vyema zaidi itakuwa,

Kila mkweza ukubwa, na yeye autamani!

 

Na ndege nayo pia, kwa papo hapo ingia,

Kwingine kutotokea, hili ukalitambua,

Zusha ya kuhurumia, usizushe ya kuonea,

Kila mkweza ukubwa, na yeye autamani!

 

Wahurumie izaya, Muumba wetu radhia,

Dhambi wanaopalilia, kwa pepo kuwaingia,

Kama kipepeo kuwa, kula bila cha kuzaa,

Kila mkweza ukubwa, na yeye autamani!

 

Umenipata ukiwa, wangu nawafikiria,

Dhehebu nalikimbia, masoni weshaingia,

Salama nawaambia, ya kwao kuwaachia,

Kila mkweza ukubwa, na yeye autamani!

 

 

No comments: