Ujinga ukisikia, ni wengine kuachia,
Wao wakajifanyia, wanayoyakusudia,
Wenyewe yakawafaa, patupu ukaambulia,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
mtakuja kwenda na maji !
Fakiri ukiambiwa, tambua walanguliwa,
Wengne kujichumia, na weye ukajikwaa,
Wao wakaendelea, nyuma wenye kubakia,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
Itakuja enda na maji !
Chini wa kukanyagiwa, hadhi mngeliijua,
Ndio juu mlokuwa, iwapo mnajijua,
Ila msipojitambua, mtazidi kuonewa,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
Mnakuja enda na maji !
Kuongoza ni hidaya, watu wakatumikiwa,
Haijawa, haitakuwa, ubaba kuuchukua,
Kisha kujiamlia, jinsi mnavyojisikia,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
Itakuja enda na maji !
Hili mkilitambua, maswali mtayazua,
Katibani kuingia, cheo mkajilindia,
Ila mkipuuzia, mwauzwa kwenye gunia,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
Mnakuja enda na maji !
KIswahili mkitumia, kila kitu mtajua,
Hata na hizo sheria, hakuna wa kupindua,
Machale
huwaambia, stopu mkendaitoa,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
Itakuja enda na maji !
Mijini mkiyajua, wenyewe mtaamua,
Huko mikoani pia, na kwenye hizo wilaya,
Uongozi mtatia, muwezao kuuchaagua,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
Mnakuja enda na maji !
Njia ya demokrasia, ni ya wengi kuamua,
Wachache wakiamua, huwa wavunja sheria,
Ni budi kuwaodnoa, wenye haki kuwatia,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
Itakuja enda na maji !
Muda itatuchukua, ila huko twafikia,
Hata wanaozuia, patupu wataambulia,
Mkiamka Tanzania, Afrika itakuwa,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
Mnakuja enda na maji !
Na
lugha hii rupia, yafaa kiuitumia,
Kanuni tukazitia, na mifumo kuizua,
Juu juu kutembea, ikatuona dunia,
Nchi hii nchi yenu, wengine mkiachia:
Itakuja enda na maji !
No comments:
Post a Comment