Mafundi wakizidisha, leseni wakazitoa,
Cheti wenzi kupandisha, na unafiki kuvaa,
Huja panako mkesha, chungu chote kufuaa,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Vyeo wanavyovikosha, kwa hisani kuzitia,
Kiasi wakazidisha, hadi wakakanyagia,
Huyatatiza maisha, na kuongeza nazaa,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Ya ovyo watayazusha, hadi vyumba vikajaa,
Kila ukikitingisha, kibiriti kinapwaya,
Huja sasa yakuwasha, kujikuna kukakua,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Mwanziishi wa rabsha, si anayekataliwa,
Ila anayetoa rushwa, ziada akajaziwa,
Siasa zikaharisha, na kwacha harufu mbaya,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Mengine ya kuchekesha, kiumbe anayozua,
Ajitikwa ya kutisha, kama kubeba dunia,
Kumbe muosha hukoshwa, bado hajayaelewa,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Angazieni maisha, haya yangu kuyajua,
Kuna mikasa yachosha, na vitendo vya
udhia,
Watu vinawewesesha, haki yao kutojua,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Mirija waiboresha, wachache kuyakamia,
Maji wakayapitisha, ya malaki sio mia,
Hali haijawawezesha, mpito utapasua,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Mita waziviringisha, maudhui kurejewa,
Hii yaanza yavusha, na nyingine zafatia,
Hilo hilo likijsaa, watu watajiepusha,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Makundi yatutingisha, yao yakikataliwa,
Nani wa kuwawezesha, ikiwa watindikiwa,
Kauli zingine zachosha, humpa mtu kuugua,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Hukuambia maisha, na lingine halijawa,
Nakataa ni kuzusha, mtakuja changanyikiwa,
Vitendo vya kubabaisha, sumu yake
kuchukiwa,
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
Tamaa lakukatisha, patupu kuambulia,
Hata kama umekesha, usambe na ya jana njaa,
Na wala hukuendesha, ila umetumikia ?
Maji yakizidi unga, ugali hugeuka uji!
No comments:
Post a Comment