Siandiki wa leo, watu wasiojijua,
Nawaandikia wajao, macho wataofungua,
Dhahiri wakaijua, na giza kuliondoa,
Haki, kweli na usawa, budi kulinda uhuru !
Havitakiwi kupungua, mizani ikitumiwa,
Kwa kadiri vyatakiwa, pasipo kufililia,
Wala ya kuongezewa, kwa kisichokusudiwa,
Haki, kweli na usawa, budi kulinda uhuru !
Haki watu kutendewa, ni dhuluma kuondoa,
Aliyeishapunguziwa, kiasi akafidiwa,
Mizani kati kukaa, kila mtu akajua,
Haki, kweli na usawa, budi kulinda uhuru !
Inapozidi hadaa, mambo itayapindua,
Kichwa chini kuja kaa, na miguu juu
kwelea,
Kinyamkela kikaa, vitu juu kusombea,
Haki, kweli na usawa, budi kulinda uhuru !
Ukweli ukiuliwa, jamii yatima huwa,
Mengi yakahasiriwa, na imani kupotea,
Na mwisho wa siku ikawa, amani imeuawa,
Haki, kweli na usawa, budi kulinda uhuru !
Hakuna aliye njia, mlango wa kupitia,
Hadi mtu kujitia, ndiyo yeye kaizaa,
Amani mama tabia, kama mbaya hupotea,
Haki, kweli na usawa, budi kulinda uhuru !
Hutoweka na kwishia, ukiwa ikawaachia,
Mkawa wa kujijua, na vijembe kufifia,
Jibari walojitia, haraka wakasinyaa,
Haki, kweli na usawa, budi kulinda uhuru !
No comments:
Post a Comment