Monday, September 23, 2013
KATIBA BILA UWAZI
KATIBA tumeamua, tunaitaka mpya,
Na hili kufanikiwa, ni lazima kuchangia,
Kila unalolijua, lawza kukusaidia,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Sera kutochakachua, kwa mifumo ya udhia,
Ikawa zinazuia, watu wetu kuchangia,
Nafasi wakatukua, kitu wasiochangia,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Usije pembeni kaa, wengine ukaachia,
Yako hawatayajua, moyoni yaliyokuwa,
Mwenyewe ukitokea, hilo litazungumziwa,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Ya zamani kupitia, ni uzuri itakuwa,
Ukapata kuijua, kasoro zilizojaa,
Nawe ukaikosoa, na kuujenga ulua,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Yafaa kufikiria, ya leo na ya kuzua,
Mbele yatayotokea, njia kuyaandalia,
Iwe si kushtukiwa, mambo yakituchachia,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Inafaa kuamua, ya wakuu wa mikoa,
Wawe ni wa kuteua, au wa kuchaguliwa,
Naona tunaumia, kwa hawa wa kuteua,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Ukubwa wauchukua, bila ya kupigania,
Wa juu wawatumia, ya kwao kufanikiwa,
Nasi katika mkoa, kitu hatutaambulia,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Kadhalika na wilaya, kama nao wanafaa,
Au wengine wakawa, kwa bora iliyo njia,
Waweze kutumikia, bila uchama kutia,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Na rais kuchagua, mikakati kuwazia,
Ni mikoa kuchagua, wasafi watu kadhaa,
Kisha wakaingia, chamani kuchaguliwa,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Ni ipi asilimia, ipate kukubaliwa,
Kidogo sana ikiwa, ridhaa inapungua,
Kubwa ikizingatiwa, bora zaidi yafaa,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Kuungana vyatakiwa, vyama hapa Tanzania,
Gharama zikapungua, lazima isiyokuwa,
Vitatu vikibakia, nafuu tutaambulia,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Na nchi kuyaamua, mbili au tatu zikawa,
Watu uhuru kuvua, ya kwao wakaangalia,
Isiwe kutawaliwa, na ndani waliokuwa,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Dola nayo kuamua, nguvu zinapoishia,
Hawa wanaotumiwa, pabaya watuchukua,
Juu wakiwa raia, nidhamuwataijua,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Mishahara twatakiwa, pia kwenda kuamua,
Vipi itakavyokuwa, utenzi kuzingatia,
Sio wanaopepewa, masultani wakawa,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Vijana tunatakiwa, uhuru kupigania,
Na sio kujatumiwa, na wazee walokuwa,
Kisha wakatuhadaa, kama panzi tulokuwa,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Kisha wakatuhadaa, kama panzi tulokuwa,
Nao kunguru wakawa, riziki wajipatia,
Nasi bila kujijua, tuzidi kuangamia,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Wazee mnatakiwa, kutumiwa kukataa,
Leo kuzungumzia, myapate manufaa,
Siasa kutowagawa, kwa vyama kuvitumia,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Wazee mkapigania, yalo yenu manufaa,
Isiwe mnatumiwa, na waliovimbiwa,
Hili mkishguhulikia, yenu yatazingatiwa,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Watoto mnatakiwa, haki zenu kuzijua,
Na kisha kushikilia, katibani kuingia,
Pasaiwe lisilokuwa, kwa vyovyote itavyokuwa,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Umoja mnatakiwa, wanawake kuulea,
Msije mkatumiwa, na wahuni walokuwa,
Nao wakishawagawa, yenu kutoangalia,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Baraka nawaombea, ndugu zangu Watanzania,
Yenu yakifanikiwa, na wangu watafanikiwa,
Nayo yakliharibiwa, nao huharibikiwa,
Uwazi unatakiwa, katiba kuichangia!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment