Monday, May 27, 2013

MWANA AKIJIFANZA BABA


Mwana cheo amepewa, na ubaba kachukua,

Sasa ataka amua, na ye akaabudiwa,

Ubaba kumnyanyua, kusiko akafikia,

Mwana akiwa ni baba, baba atakuwa mwana ?

 

Baba aliposinzia, kakuta kahujumiwa,

Mwana kitini kakaa, na ukubwa kujitia,

Subira inatakiwa, sio baba kumwambia,

Mwana akiwa ni baba, baba atakuwa mwana ?

 

Haki hajatutendea, ya kwetu kuyavamia,

Cheo alichopewa, ubaba hakijamwachia,

Ubaba unabakia, wananchi wa Tanzania,

Mwana akiwa ni baba, baba atakuwa mwana ?

Kawaida inakuwa, mwana kazi kulelewa,

Akishapiga hatua, hekima akaijua,

Ndipo anapoachiwa, mengine kushughulikia,

Mwana akiwa ni baba, baba atakuwa mwana ?

 

Mwana ndio anakuwa, ukubwa ang'ang'ania,

Nchi chini juu yawa, na mengi kuhujumiwa,

Kisa kinachotokea, mwana nchi keshapewa,

Mwana akiwa ni baba, baba atakuwa mwana ?

 

Uttoo bado wanukia, vipi atayoamua,

Sana hujipendelea, chote akajimegea,

Chakula tukaishiwa, tubaki kupigania,

Mwana akiwa ni baba, baba atakuwa mwana ?

 

Nidhamu ataka pewa, na utu kuutambua,

Dunia hii ni njia, si pahala pa kukaa,

Katika kujipitia, wote wakaangaliwa,

Mwana akiwa ni baba, baba atakuwa mwana ?

 

Heshima inatakiwa, kwa wa juu na chini pia,

Kule unakopuuzia, ndiko nyufa hutukia,

Birika tundu kitiwa, kamwe haiwezi jaa,

Mwana akiwa ni baba, baba atakuwa mwana ?

 

Majidi twamwachia, macho akawafungua,

Ukweli wakatambua, na kujirudi tabia,

Wakiivunja ubia, na hisani hupotea,

Mwana akiwa ni baba, baba atakuwa mwana ?

 

 

Kulinda uhuru


Siandiki wa leo, watu wasiojijua,

Nawaandikia wajao, macho wataofungua,

Dhahiri wakaijua, na giza kuliondoa,

Haki, kweli na usawa, budi kulinda  uhuru !

 

Havitakiwi kupungua, mizani ikitumiwa,

Kwa kadiri vyatakiwa, pasipo kufililia,

Wala ya kuongezewa, kwa kisichokusudiwa,

Haki, kweli na usawa, budi kulinda  uhuru !

 

Haki watu kutendewa, ni dhuluma kuondoa,

Aliyeishapunguziwa, kiasi akafidiwa,

Mizani kati kukaa, kila mtu akajua,

Haki, kweli na usawa, budi kulinda  uhuru !

 

Inapozidi hadaa, mambo itayapindua,

Kichwa chini kuja kaa, na miguu juu kwelea,

Kinyamkela kikaa, vitu juu kusombea,

Haki, kweli na usawa, budi kulinda  uhuru !

 

Ukweli ukiuliwa, jamii yatima huwa,

Mengi yakahasiriwa, na imani kupotea,

Na mwisho wa siku ikawa, amani imeuawa,

Haki, kweli na usawa, budi kulinda  uhuru !

 

Hakuna aliye njia, mlango wa kupitia,

Hadi mtu kujitia, ndiyo yeye kaizaa,

Amani mama tabia, kama mbaya hupotea,

Haki, kweli na usawa, budi kulinda  uhuru !

 

Hutoweka na  kwishia, ukiwa ikawaachia,

Mkawa wa kujijua, na vijembe kufifia,

Jibari walojitia, haraka wakasinyaa,

Haki, kweli na usawa, budi kulinda  uhuru !

 

 

Monday, May 13, 2013

Upofu wa roho na moyo

WENGI hutatizika, upofu kiwaingia,
Roho ikadahaika, kwa upofu kuivaa,
Mengi sana kutamka, kwa ulimi kupotoa,
Mtu kipata upofu, irejee roho yako !

Moyo unaghilibika, kwa kutafuna tamaa,
Joho silo kujivika, lifaalo kuvaliwa,
Nafsi kutaabika, lawama inayojua,
Kitu ki'kupa upofu, udhibiti moyo wako !

Kimali nafilisika, ila roho yanambia,
Ukwasi umeishika, yanitaka kutulia,
Tena kutohangaika, lijalo kulingojea,
Mtu kipata upofu, irejee roho yako !

Vipofu wakiiongoka, na viziwi kusikia,
Taharuki wakataka, na hatua kuchukua,
Na ngao zikatumika, kama kinga kuzuia,
Kitu kitia upofu, udhibiti moyo wako !

Yawezayo kuwafika, mbali wakafukuzia,
Wenye tamaa  kuzika, sahau ikaingia,
Na wanaostahika, umma wakaangalia,
Mtu kipata upofu, irejee roho yako !

Hofuni wenye shirika, yao wanayoyazua,
Uchu unapowashika, hadi watume wakawa,
Na vyeti wakavipoka, na utu kuuhadaa,
Kitu kitia upofu, udhibiti moyo wako !


Kwa nyuma wakiwapoka, na mbele kuwagawia,
Wanafiki wastahika, kuangalia yafaa,
Wana yao wayashika, sio yenu kuyajua,
Mtu kipata upofu, irejee roho yako !

Watu hawa wa mashaka, ndio waliosambaa,
Njia zote wazifika, wapitao kuwavaa,
Lao halijagungulika, na wengi wapopolewa,
Kitu kitia upofu, udhibiti moyo wako !

Zao zinasambazika, mifuko yafunguliwa,
Ili mpate tatizika, na wehu mkaingia,
Ikawa mnaotamka, lile msilolojua,
Mtu kipata upofu, irejee roho yako !

Ikawa mwahamanika, kimakosa kuamua,
Ibilisi kumshika,Mola mkamuachia,
Kisha aje kuwazika, ilhali mwapumua,
Mtu kipata upofu, irejee roho yako !

Yangu kuja kutajika, hali mmeishapotea,
Na nchi kuhairibika, na watu wakalaniwa,
Usiya asiyeushika, hedaya yake balaa,
Kitu ki'kupa upofu, udhibiti moyo wako !




Monday, April 29, 2013

Sunday, April 21, 2013

Nyumba isiyo na haki


Nyumba ikosayo haki, baba huwa mnafiki,

Limbwata ikimwashiki, ya wana hatoafiki,

Akaachia mikiki, rabsha na taharuki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

Biblia hutaliki, na Daudi hasemeki,

Qurani haifunguki, ya Selemani kucheki,

Akili zao riziki, na kisha umamuluki,

Nyumba isiyo na haki, maisha haijengeki!

 

Wangeata unafiki, mistari ina haki,

Wasingejaribu hiki, hofu ingetamalaki,

Ujinga wauafiki, dunia haisomeki,

Nyumba isiyo na haki, milele haisimamiki!

 

Nyumba ikosayo haki, baba huwa mnafiki,

Limbwata ikimwashiki, ya wana hatoafiki,

Akaachia mikiki, rabsha na taharuki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

Nuru haimpeleki, na aendako haafiki,

Katikati huafiki, akakwaza ushtaki,

Akawa haaminiki, na leke halithaminiki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

Huzaa huambiliki, na mkubwa unafiki,

Ya usawa na ya haki, yawe kwake hayasikiki,

Wakasepa washtaki, yawe hayaeleweki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

Ya haki akataliki, na kuikwaza milki,

Baraka ikahamaki, na hekima kuishtaki,

Ukazuka umamluki, pia nao uzandiki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

Nyumba isiyo na haki, wevi wataibariki,

La kweli halitamkwi, na uongo huafiki,

Wema ukawa kisiki, waovu hawautaki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

Umma huudhhaki, yeye ndio mwenye haki,

Kusema wasidiriki, wanaihofia dhiki,

Ila wakitaharuki, nao huja kuhamaki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

Huukataa uzandiki,  na kubwaga unafiki,

Wakaililia haki, kila kona kutamalaki,

Ukaisha umamluki, kwa kumhofu Maliki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

Nyumba yetu ibariki, ewe bwana mtoa haki,

Hakikisha hawafiki, wote wenye unafiki,

Kiwatibue kisiki, wawe juu hawaamki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina amani!

 

Huzaa huambiliki, na mkubwa unafiki,

Ya usawa na ya haki, yawe kwake hayasikiki,

Wakasepa washtaki, yawe hayaeleweki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

Madaraka  huwanoki, injini haziamki,

Ya mwana hawashtuki, ila yao huhamaki,

Usanaa huulaki, sera wakaiafiki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina amani!

 

Umma huudhhaki, yeye ndio mwenye haki,

Kusema wasidiriki, wanaihofia dhiki,

Ila wakitaharuki, nao huja kuhamaki,

Nyumba isiyo na haki, huwa haina imani!

 

 

Tuesday, April 9, 2013

SHETANI WA NA MIMI NICHINJE !


 

Shetani wa na mimi nichinje

 

ASILI tunaijua, itokako Tanzania,

Mababu waliamua, nani wa kutuchinjia,

Mwaikana historia, na utu kuuchezea?

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Tuliungana jamii, nasara na islamiya,

Ndugu tukawaachia, kazi ya kutuchinjia,

Mbegu tukiitambua, Ibrahimu kuanzia,

Shetani 'nami' nichinje, ashindwe na alegee!

 

Yaliyoishaamuliwa, vipi twaja yafukua,

Makaburi kuyazua, walo hai kuwatia,

Au mnalololijua, sisi bado kulijua?

Shetani 'nami' nichinje, ashindwe na alegee!

 

Yapo ya kuzungumzia, nchi ikaendelea,

Barabara zatakiwa, vijijini kuingia,

Na madaraja kuzua, watu wakajivukia,

Shetani 'nami' nichinje, ashindwe na alegee!

 

Mashamba yanatakiwa, kulima kulisha Tanzania,

Na kiasi kuongezea, dunia kuiuzia,

Kuchinja twapigania, hivi kweli twajijua?

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Hivi kweli twajijua, kwa tunayojisemea,

Au wehu watuingia, ya ovyo kujiamlia,

Dunia kutushangaa, mfano  tuliokuwa?

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Mengi tungelifikiria, ubora kujiongezea,

Afrika kutambua, ni darasa tumekua,

Sisi tukatangulia, na wengine kufatia,

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Ya wa Kongo twaamua, sasa kwenda kurejea,

Kwanza tungejichungua, kama wazima raia,

Au tumeingiliwa, na walio ni vichaa,

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Burma ukiangalia, kichaa kajizukia,

Ndugu anawachukia, na uadui kuwatia,

Hivi sasa awaua, na nyumba kuwaunguzia,

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Iraqi na Syria, dini zinahujumiwa,

Wauana raia, kwa hata wasiyojua,

Ni vichaa wamekuwa, nchi zinateketea,

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Amiri anatakiwa, katikati akakaa,

Mstari kuutia,  hakuna wa kuuchezea,

Maaamuzi yatakiwa, sio lawama kutoa,

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Maji yanatusumbua, lazima kujivunia,

Majumbani kuingia, na mashambani kumwaa,

Kuchinja wito likiwa, naona tunafulia,

Shetani 'nami' nichinje, ashindwe na alegee!

 

Kongo wanatungojea, kwenda kuwahubiria,

Nchi ya kati nayo pia, uamsho yangojea,

Kimataifa tukiwa, thumni hatutapigania,

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Masoko kujitafutia, nyie mngetangulia,

Wafuasi kufatia, sadaka wakajipatia,

Michango yao ikawa, na nchi kwenda chanua,

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

Nchi ninaiombea, kuvuka hii balaa,

Kwa uongo kukataa, na ukweli kulilia,

Salama ya Tanzania, sote yatutegemea,

Shetani 'nami' nichinje, adhindwe na alegee!

 

ISIWE MIAKA HII NUHUSI !!!

 
Wakuu twawaambia, juu walioshikilia,
Macho yao kufungua, kujua kinachoendelea,
Wapunguze kusinzia, hali watu wauawa,
Isiwe miaka hii, ya  historia nyeusi!
 
Awamu iloanzia, ndiyo inaendelea,
Urafiki ilizua, hadi mitano kwishia,
Kipindi kilofatia, ajabu zikazuliwa,
Isiwe miaka hii, ni ya umwagaji damu!
 
Kubenea kuanzia, asidi akamwagiwa,
Hadi leo analia, mbaya hajamjua,
Na wala hatujasikia, kama kapewa fidia,
Isiwe miaka hii, ya  historia nyeusi!
 
Mwangosi akafatia, mchana akauawa,
Wakubwa wafatilia, hadithi hatujaijua,
Na bado hatujajua, wana kulipwa fidia,
Isiwe miaka hii, ni ya umwagaji damu!
 
Absalom kafatia, hadi uchongo kutiwa,
Uchunguzi waendelea, mwisho tutajionea,
Hekaya itayokuwa, ni rahisi kung'amua,
Isiwe miaka hii, ya  historia nyeusi!
 
Umoja unatakiwa, mafia wameshaingia,
Waliko kuwafichua, na kubwa ni yao nia,
Nini wanaitakia, hii yetu Tanzania?
Isiwe miaka hii, ni ya umwagaji damu!
 
Waandishi mwatakiwa, ya kwengu kufatilia,
Ukweli mkaujua, ili kinga kuitwaa,
Mkiwa mwaangalia, kulia huwa tabia,
Isiwe miaka hii, ya  historia nyeusi!
 
Haraka mnatakiwa, mitandao kuizua,
Nchi mkaichungua, na wabaya kuwajua,
Kama ni hongo wapewa, na nyie si mnayajua?
Isiwe miaka hii, ni ya umwagaji damu!
 
Huenda ndani kakaa, mbaya msiyemjua,
Au mahala katulia, kimulimuli akawa,
Mbele anatangulia, mumiani kufatia,
Isiwe miaka hii, ya  historia nyeusi!
 
Ili nchi kuokoa, wamulikeni mafia,
Nchini walioingia, kuharibu Tanznia,
Mhanga kujitolea, salama wana kukaa,
Isiwe miaka hii, ni ya umwagaji damu!
Isiwe miaka hii, ya  historia nyeusi!
 
Huhalalisha kuua, ili cheo kupatiwa,
Au fedha kuzikwaa, kisha wakazichezea,
Yafaa kujiokoa, kwa wao kuwatambua,
Isiwe miaka hii, ya  historia nyeusi!
 
 
Mungu hawakujaliwa, shetani waabudia,
Ndivyo inavyokuwa, na roho wasiojaliwa,
Fisadi huabudia, ukuu sio raia,
Isiwe miaka hii, ya  historia nyeusi!
 
Twawaomba waheshimiwa, doa hili kulitoa,
Nchi inahujumiwa, kwa kuwa na sifa mbaya,
Tujali demokrasia, na uhai kwangalia,
Isiwe miaka hii, ya  historia nyeusi!