Monday, August 26, 2013

HASARA KUBWA KWA N CHI


Rahisi kununuliwa, mfukoni akatiwa,
Kisha akajatumiwa, mwenyewe kuja jiua,
Hajui anachojua, msukule keshakuwa,
Hasara kubwa kwa nchi, kijana asojijua !


Atafuta ganga njaa, sio kiongozi kuwa,
Dhiki akaiondoa, katikati amekaa,
Wabaya  kuwaondoa, watu wanaonunua,
Hasara kubwa kwa nchi, kijana asojijua !

Kujiamini silaha, yeye asiyochukua,
Kubebwa keshazoea, kila kitu hufanziwa,
Kutafuta hatajoua, sikuzote wa kupewa,
Hasara kubwa kwa nchi, kijana asojijua !

Huiabudu dunia, Mola akamkimbia,
Upepo akishatiwa, akazidi kuvimbiwa,
Hadi juu hujaa, kwenye anga akapaa,
Hasara kubwa kwa nchi, kijana asojijua !

Hapo anapofiikia, Mungu huja jidhania,
Wahyi akautoa, kwa amri zisokuwa,
Hajui la kutumiwa, wala la kufikiria,
Hasara kubwa kwa nchi, kijana asojijua !

Kiatu husiginia, watakaomsaidia,
Akili akadhania, pekee amejaliwa,
Kumbe hajajijua, kubaya aogelea,
Hasara kubwa kwa nchi, kijana asojijua !


MWENYE KUTOA KWA DHATI


HATAKI kuangaziwa, sadaka akiitoa,
Kwenye siri huingia, Molawe kumuachia,
Viumbe kutotegemea, kitu kumsaidia,l
Mwenye kutoa kwa dhati, tivii huiogopa!

Uungu huukimbia, na riziki kuzigawa,
Apendwaye akapaewa, asopendwa kuchukiwa,
Riziki akakatiwa, na matatani kutiwa,
Mwenye kutoa kwa dhati, gazeti huliogopa!

Mola humtangulia, afaaye ogopewa,
Ndiyo wa kutetemekewa, milki anayegawa,
Na ukuu kuwagiwa, wale anaochagua,
Mwenye kutoa kwa dhati, inteneti huogopa!

Mitihani aijua, kunaguka huhofia,
Asije kuteketea, badala kujiokoa,
Waliomtangulia, zao keshaelezewa,
Mwenye kutoa kwa dhati, redio huzikimbia!

Nafsi aitambua, ilivyojaa hadaa,
Uungu ikalilia, japo kifo chaingojea,
Ila uhai ukiwa, kila kitu hugombania,
Mwenye kutoa kwa dhati, tivii huiogopa!

Kazi moja aijua, mbingu zinaiongojea,
Ibada ya kutulia, na kisha kusaidia,
Kwa faragha kuamua, na kutenda vivyo pia,
Mwenye kutoa kwa dhati, gazeti huliogopa!

Hatonjojea mataa, na kamera  kuletwa,
Dunia ipate mjua, ni nani aliyetoa,
Kwani anatambua, walipaji hawajawa,
Mwenye kutoa kwa dhati, inteneti huogopa!

Mlipaji katulia, yeye ajitazamia,
Malaika wahadithia, viumbe zao tabia,
Taarifa huletewa, wa kweli wakawajua,
Mwenye kutoa kwa dhati, redio huzikimbia!


mtu asiyejijua

Vyovyote anatumiwa, na wengine kuwafaa,

Yeye kama chombo huwa, mashinani kusagiwa,

Mtu kutojitambua, utumwa kwake tabia!

 

Hushindwa 'jifikiria, sembuse kufikiria?

Kama vile ndoo kuwa, au karai kutumiwa,

Zege akalichangia, pasina na sifa kuwa,

Mtu kutojitambua, utumwa kwake tabia!

 

Dezo atanunuliwa, na walionunuliwa,

Mfukoni akatiwa, ndivyo sivyo kutumiwa,

Vishilingi akipewa, tajiri akajisikia,

Mtu kutojitambua, utumwa kwake tabia!

 

Kwa cheo huzainiwa, hata wana kuwaua,

Ukuu akauwania, kwa damu kujimwagia,

Hesabu akijaijua, hubaki kujijutia,

Mtu kutojitambua, utumwa kwake tabia!

 

Mara huchanganyikiwa, misuli kuitanua,

Kisha akaazimia, kuikusanya dunia,

Hajui hatobakia, dunia kumngojea,

Mtu kutojitambua, utumwa kwake tabia!

 

Miaka keshahesabia, kisha motoni kwingia,

Milele kwenda kukaa, kwa anayoyamua,

Laiti angetambua, vivyo  asingetumiwa,

Mtu kutojitambua, utumwa kwake tabia!

 

Roho inapotolewa, ndio ukweli hujua,

Tena sana akalia, dakika kuruhusiwa,

Mema akachangia, moto kwenda ukimbia,

Mtu kutojitambua, utumwa kwake tabia!

 

Rushwa hutaka kutoa, malaika kugawia,

Wapate kumuachia, dakika akasalia,

Ila hatohurumiwa, macho akayakodoa,

Mtu kutojitambua, utumwa kwake tabia!

 

Huwezi kuwazaini



KUWA bingwa wa hadaa, na kofia kuzivaa,

Kamwe hautojaliwa, wote wakakusikia,

Lako kulihudumia, ukweli ukauawa,

Huwezi kuwazaini, watu wote, pande zote!

 

Idadi hutachukua, ya bure na kununua,

Ndicho tulichoumbiwa, viumbe tuliopotea,

Utumwani hujitia, wenyewe kwa kuchagua,

Huwezi kuwazaini, watu wote, rika zote!

 

Kamba huwa ni hidaya, mkononi kuzitia,

Kisha kujitundukia, tunapoamriwa,

Amri kuzisikia, hata zilizo ukiwa,

Huwezi kuwazaini, watu wote, siku zote!

 

Hatuwi wa kuchagua, ya kwetu kufikiria,

Kubebwa tumezoea, hatutaki kutembea,

Kiyama kinatujia, hali twakiangalia,

Huwezi kuwazaini, watu wote, pande zote!

 

Twashindwa kuyaamua, ya kwenda kutuokoa,

Firdausi kuingia, pepo ya kuteuliwa,

Mithili isiyokuwa, wala haitatokea,

Huwezi kuwazaini, watu wote, rika zote!

 

Twashndwa kujichagua, vikongwe kukimbilia,

Mikongojo sisi kuwa, badala ya kujisimamia,

Ushauri nautoa, bongo zetu kufungua,

Huwezi kuwazaini, watu wote, siku zote!

 

Bongo zetu kufungua, kofuli kuziondoa,

Funduo kuzitumia, Mola keshatupatia,

Njia mkishahofia, mbele kutoendelea,

Huwezi kuwazaini, watu wote, pande zote!

 

Msije kuyayatuia, kwamba haya mliambiwa,

Nanyi hamkusikia, dhihaka mkaitia,

Wa kweli anayejua, pande hatoegemea,

Huwezi kuwazaini, watu wote, rika zote!

 

Rabuka namsifia, itihari kujaliwa,

Kweli nikapigania, na haki kuigombea,

Japo fakiri nikiwa, ikawa yangu ridhaa,

Huwezi kuwazaini, watu wote, siku zote!

Friday, June 28, 2013

Raia si watoto




Wanalosema wajua, sio wa kutamkiwa,
Watendalo waelewa, sio wa kuelezewa,
Vingine ikitokea, lawama mwajitakia,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Hawajaugua kichaa, na kamwe sio majuha,
Wana lao wakilia, kusikizwa watakiwa,
Vingine inapokuwa, mwaendeleza udhia,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Hata wasiobukua, na elimu kuzivaa,
Majoho kuning'inia, na kupambwa na kofia,
Kichwa tupu walokuwa, haki zao wazijua,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Wafaragua sanaa, na vitendo maridhia,
Visivyoleta ukiwa, na jeraha kuwatia,
Adili ikisinyaa, kimya wategemea?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Hali wanajionea, ghali bure kusifiwa,
Lao wanalolijua, gharama zawalemea,
Hivi waache kulia, sawa mtajionea?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Tofauti zinakua, hakuna la kuzuiwa,
Wa juu waogelea, chini wazama dhiraa,
Sera zimetibuliwa, nani kuwasaidia ?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Kila aliyejaliwa, azidi kuongezewa,
Na yule asiyekuwa, alichonacho mwataa,
Wapi pa kuegemea, ikasikia dunia?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Utundu mwawazuliwa, na ukaidi kuwatia,
Ya kwenu mpate zua, kuezuka na kuezua,
Nani wa kuangalia, ya kwao yaliyokuwa?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Hamaki mnajitia, na vitisho kuvitoa,
Ndimi zinawalemea, madhambi yawachefua,
Nani ni wa kutubia, wakuu au raia?
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Vitabu mngefungua, adili mkaijua,
Ukweli mlioua, uanze tena chanua,
Haki mlojizikia, muanze kuzifufua,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Muikomeshe hadaa, na wengine kuonea,
Kwa kuwa mmejaliwa, si wengine kushindiliwa,
Dhuluma huja umbua, haki ikijifungua!
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Kila mwenye kujua, ishara huziagua,
Za wakati zilokuwa, ya kale akaachia,
La, hasha akiendelea, yake huja muumbua,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Ninachowaambia, wakati umewadia,
Mseto kufikiria, mkaepusha balaa,
Imla mkidandia, mtashuka kati ya njia,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

Vyote mnang'ang'ania, wenzenu wataridhia?
Kidorik uwaachia, hata kidunchu kikiwa,
Hili msipotambua, uchawi mwaununua,
Raia sio watoto, ni watu na heshima zao!

YALIYOTOKEA PARIS


Wale waliojaliwa, kila kitu walitwaa,

Wakawa wang'ang'ania, kidunchu kutoachia,

Hoja wakazikataa, ndani kujitomelea,

Paris yalitokea, someni historia!

 

Tofauti zilokuwa, ni bomu waliambiwa,

Wao wakajitetea, ubepari ndio dawa,

Nusura hawakuamua, kilichobaki balaa,

Paris yalitokea, someni historia!

 

Bepari wakaamua,  vya dola kuvitumia,

Nchi ikagugumia, kwa kilio kuzuiwa,

Hadi yalipotokea, yale yasiyotarajiwa,

Paris yalitokea, someni historia!

 

Wasio nacho walia, mwneye nacho agomea,

Wingi wakautumia, ya kwao kujipatia,

Nani angewazuia, kadari kuiondoa?

Paris yalitokea, someni historia!

 

Wote walisanzulia, tena pasina silaha,

Unyongaji kuenea, Ufaransa ilokuwa,

Waloshiba kuwaniwa, kila walipokikaa,

Paris yalitokea, someni historia!

 

Paris ikajillia, hatima iliyozua,

Bepari kuondolewa, ukaingia ujamaa,

Haki ikapiganiwa, mwishowe kujisimamia,

Paris yalitokea, someni historia!

 

Muafaka nawambia, somo hili kutumia,

Huko tunakoelekea, giza ninajionea,

Kama hamtanisikia, itajaza historia,

Paris yalitokea, someni historia!

TUTUMIENI NADHARI



Wa dini pia siasa, tujifunzeni hadhari,

Ya jana si ya sasa, yameingia shubiri,

Na kwetu kubwa fursa, ni kuepusha hatari,

Tujifunzeni nadhari, viongozi Tanzania!

 

Tujipigeni msasa, kuziepusha hatari,

Na kukosa sio kosa, kosa ni kulikariri,

Maisha yasiwe mkasa, tuitumie nadhari,

Tujifunzeni nadhari, viongozi Tanzania!

 

Hakuna wa kumsusa, na kujitia kiburi,

Lazima kujitakasa, kwa wabaya na wazuri,

Vingine tukijinesa, ya heri huwa ya shari,

Tujifunzeni nadhari, viongozi Tanzania!

 

Hili adhimu darasa, maisha kutafakari,

Tukateta na kunasa, wapi tunakoabiri,

Ikiwa tunajitosa, kubaya tukahadhari,

Tujifunzeni nadhari, viongozi Tanzania!

 

Wa Yesu au Issa, wote tujenge hadhari,

Nchi isiwe ni tasa, kwenye kuzua ya kheri,

Hii ni njema fursa, kingine tusisubiri,

Tujifunzeni nadhari, viongozi Tanzania!

 

Tuufungue kurasa, wa nchi yenye hadhari,

Kujua iwe yapasa, njia yetu kukariri,

Tukaikuza hamasa, kwenye bora ushauri,

Tujifunzeni nadhari, viongozi Tanzania!

 

Msikiti na kanisa, wkaawa ni washauri,

Kila jema tukinusa, kugawa iwe ni kheri,

Ubinafsi kuususa, unazo kubwa hatari,

Tujifunzeni nadhari, viongozi Tanzania!

 

Mola hawezi kutosa, mkusanyiko wa kheri,

Kati yetu atadesa, huyo mwingi wa Saburi,

Utaifa ukanasa, nasi kuvuna mazuri,

Tujifunzeni nadhari, viongozi Tanzania!