Monday, January 28, 2013

WAPENZI KUCHUKIANA...


Wawili wanaopendana, wakaacha aminiana,

Wivu ukagandamana, na hofu ya kuumizana,

Hufariki muamana, iwe  kama ni laana,

Wajapokuchukizana, wapenzi huchukiana!

 

Huisha kuaminiana, watu wakahofiana,

Ikawa ni kuwindana, kwa usiku na mchana,

Raha wakawa hawana, ila ya kuchunguana,

Wajapokuchukizana, wapenzi huchukiana!

 

Zama waliokipatana, wakawa si waelewana,

Shere wameshachezana, mashavu wanuniana,

Na mioyo inapindana, ubaya kutakiana,

Wajapokuchukizana, wapenzi huchukiana!

 

Mahaba walopeana, sumu wakamwagiana,

Na nje kukashifiana,ya ndani kufichuana,

Siri pakawa hakuna, kila kitu ni bayana,

Wajapokuchukizana, wapenzi huchukiana!

 

Haya watatenguana, na udhu kukatazana,

Mbio wakatimuana, kwenda wasikotakikana,

Dunia ikawaona, sio watu wa maana,

Wajapokuchukizana, wapenzi huchukiana!

 

Sura watachafuana, zikawa tambo hazina,

Soni zikawa ni suna, paisna kuhifadhiana,

Wchache wakulingana, katu kutotokezana,

Wajapokuchukizana, wapenzi huchukiana!

 

Dira huharibiana, ziishe kupindana,

Mbele sasa kutoona, wawe wanaangaliana,

Huruma wakawa hana, na utu waozeana,

Wajapokuchukizana, wapenzi huchukiana!

 

Wakawa wa kushindana, ubaya kufanyiana,

Muafaka kuzozana, waaswapo kupatana,

Lengo wakawa hawana, wakabaki madubwana,

Wajapokuchukizana, wapenzi huchukiana!

 

Binadamu muungwana, haya anapoisana,

Na huruma kutona, kwa marefu na mapana,

Vingine ya binti suna, hayawani humuona,

Wajapokuchukizana, wapenzi huchukiana!

 

UNACHOKITEGEMEA


Kinaweza kupotea, tena kutokujionea,

Ukabakia mkiwa, daima wewe kulia,

Na kurudi sio njia, huyoyoma na kwishia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Leo unakiringia, kesho utakililia,

Kisha ukaugilia, asante hukuitoa,

Shere ulikichezea, na dosari kukitia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Ujivuni ukavia, na kukushuka kifua,

Haya ukaisikia, wengi ulivyonyanyapaa,

Ukajuta kwa kinaya, tena hutojionea,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Wote uliowaambaa, hutamani kurejea,

Na wasiojitambua, mtego wataingia,

Ila kwa wenye kujua, mbali sana watakaa,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Nafasi hukuachia, upate vema pumua,

Njia wakaifagia, pasina kuitumia,

Milango wakifungua, ndani patupu pakawa,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Macho watayachezea, kama makengeza kuwa,

Na duara kuyatia, kama Kipanya wakawa,

Mchoro ukaujua, ni katuni maridhiwa,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Katika hii dunia, hupewa na hutwaliwa,

Tayari unapokaa, hili utaling'amua,

Vyote aushi si nia, huja vikajiondokea,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Nipe ridhiko Jalia, kwa kuwa na kutokuwa,

Ikawa kwa historia, utawa ninaujua,

Ubora uliokuwa, ni kwa vyote kuachia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Nisiwe wa kubomoa, patakapo kukamua,

Jiwe kutokaribia, maziwa halitatoa,

Katiti nilichopewa, nizidi kuangalia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Nisiwe kung'ang'ania, pale nisipotakiwa,

Kila anayechanua, thamani hujikuzia,

Sina la kuongezea, siidanganyi dunia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Hapo nilipofikia, mbele sintoendelea,

Yangu yamehasabiwa, zaidi haitakuwa,

Mwalimu niliyekuwa, mwanafunzi ninakuwa,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Naenda tafuta njia, upenyoni kupitia,

Nusura kuifichua, tunduni iliokotiwa,

Mimi nikaichukua, mkononi kuitia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

DUA ZETU HUWA DAWA...


Ninaianza tasua, kwa pazia kulitoa,

Jalali kaniridhia, shukrani ninatoa,

Siye niliyeanzia, karne zimeshatimia,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

 

Viumbe hujifutua, uovu kuparamia,

Kama mipira ikawa, kudunda watarajia,

Ya watu huwazuzua, pabaya wakaingia,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

 

Chini wanapoanzia, hudhania ni wakiwa,

Juu wakishafikia, pumzi huzitanua,

Fahari wakatamia, na kiburi kukitia,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

 

Ujibari ukakua, ya Mola kuyachezea,

Visa mkasa ikawa, kwao ndio mazoea,

Ila siku hufikia, ukweli wakaujua,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

 

Ila siku hufikia, ukweli wakaujua,

Hasa wanapoingia, imani iliyowakaa,

Mukubuli yao kuwa, yasiache kupokewa,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

 

Uchamungu ukitua, meseji haitapotea,

Wenda inapotakiwa, kwa wakati kuingia,

Ikajionea dunia, ujumbe wakaujua,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

 

Majina yetu bandia, kwa mengi sana twapwaya,

Vitabu twaviambaa, na dua kutozijua,

Nazo ibada kadhaa, zingine zinapotea,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

 

Wakati umewadia, Yarabi kumrejelea,

yake tukasimamia, na hali njema ikawa,

Pamwe naye tutakuwa, bishara tukizitoa,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

 

Nyakati zajifungua, sana wazi zinakuwa,

Gizani tuliyokuwa, mwanga sasa waingia,

Efemu kiifungua, chuoni unaingia,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

 

Daraja unayetoa, hadh yetu angalia,

Shere wanaokusudia, mkengeni kuwatia,

Kamba umetupatia, tuwezeshe kutumia,

Dua zetu huwa dawa, uchamungu ukiwepo!

Mtu akistuliwa....


Mola anayemridhia, hakosi kumgutua,

Kisa kinapotokea, akawa mwenye kujua,

Toba inayongojewa, si ile ya kutania,

Mtu akistuliwa, haachi kujitambua !

 

Hadharani hutokea, pasina kawa kutiwa,

Watu wakajionea, na ishara kuijua,

Yapo ya kuyachezea, mengine ni kujiua,

Mtu akistuliwa, haachi kujitambua !

 

Maumbile huacha, kazi yakajifanzia,

Vifua ikakunjua, hisia kuzielewa,

Kila asiyelaaniwa, tanzu akazitambua,

Mtu akistuliwa, haachi kujitambua !

 

Katika hii dunia, michache inabakia,

Anayejielewa, ajua la kuamua,

Anayezuzuliwa, hubakia kuchezea,

Mtu akistuliwa, haachi kujitambua !

 

Kinyago huchukuliwa, hadhiye anayopewa,

Mola akampatia, kambaye kuning'inia,

Akija kushtukia, wasaa unshawadia,

Mtu akistuliwa, haachi kujitambua !

 

Vidole huvitanua, alama akavitia,

Kisha vikakunjuliwa, ufahamu kuutia,

Kula mwenye kujaliwa, adhana akasikia,

Mtu akistuliwa, haachi kujitambua !

 

Kazi tunazojipea, daraja zinapungua,

Ila kwa kutokujua, bora tunazidhania,

Shetani akatuvaa, tukashindwa kuachia,

Mtu akistuliwa, haachi kujitambua !

 

Shehe Ali alijua, aweza kusimulia,

Baraza wakaikaa, na hali kuangalia,

Vingine vinavyotokea, vyawasuta wasokuwa,

Mtu akistuliwa, haachi kujitambua !

 

Namshukuru Jalia, fikra kunijalia,

Kuwaza na kuwazua, na wengine kumegea,

Uchoyo sikujaliwa, japo tajiri sijawa,

Mtu akistuliwa, haachi kujitambua !

Saturday, January 26, 2013

Aliyekutangulia



AJABU itatokea, wewe uliyefuatia,

Kidomo ukajitia, kwa alotangulia,

Uapizo kuutia, eti kwani wachukia,

Aliyekutangulia, waweza kumuapiza ?

 

Kama panao ubaya, mukubuli huwa dua,

Ila onyo ukipewa, watakiwa lichukua,

Vingine ukiamua, madhila unajitia,

Aliyekutangulia, waweza kumuapiza ?

 

Leo hutofikiria, hadi kesho ikiingia,

Ikawa umechelewa, yakufika yametua,

Na hii ndiyo dunia, ilivyo yake tabia,

Aliyekutangulia, waweza kumuapiza ?

 

Subira ukiijua, neno utalifatia,

Kisha ukalichimbua, na  mizizi kuing'oa,

Kama mhogo kuliwa, na sumu  kuondolewa,

Aliyekutangulia, waweza kumuapiza ?

 

Pepo katika dunia, huwa zina ya kuzua,

Hasa zikakurubia, tanga kwenda zisumbua,

Na vyombo vikaelea,  kule visikotakiwa,

Aliyekutangulia, waweza kumuapiza ?

 

Wengi yamewazuzua, bora wakayaachia,

Haraka kukimbilia, ziliokofika tamaa,

Wakija kujigundua, wakabakia kulia,

Aliyekutangulia, waweza kumuapiza ?

 

Vibaka kwenye dunia, daraja walishapewa,

Wa chini hutuhunia, wa juu twawachukua,

Pasina sisi kujua, mijitumwa kubakia,

Aliyekutangulia, waweza kumuapiza ?

 

Yao yakatengamaa, na yetu tukafulia,

Na saa ikiwadia, litafunguka pazia,

Nje tukajionea, sivyo ilivyotakiwa,

Aliyekutangulia, waweza kumuapiza ?

Tambiko likiondoka



KAMA mbuyu na mkuyu, tambiko lilipokaa,

Watu huja kwa miguu, kuja soma zao dua,

Kafara wasisahau, mashinani kuzitoa,

Tambiko likiondoka, koo husambaratika !

 

Wazazi huyanukuu, mila zikafuatia,

Wakarithi wajukuu, na kizazi kwendelea,

Kwa gharama na nafuu, hakuna wa kuchimbua,

Tambiko likiondoka, koo husambaratika !

 

Wazima nao mafuu, kuuuliza hukataa,

Wakahofu ubahau, kizazi kutunukiwa,

Au ya koo dharau, na wengine kuchukia,

Tambiko likiondoka, koo husambaratika !

 

Lilipo ni sikukuu, hadi likijang'olewa,

Pakabaki kichuguu, mchwa kwenda kuhamia,

Yakaanza mahuruhu, makaburi kufagia,

Tambiko likiondoka, koo husambaratika !

 

Moyo wangu ni juzuu, hapa nilipofikia,

Hakijaja kitukuu, na sijaijua dunia,

Na sijda na rukuu, wala hazijatimia,

Tambiko likiondoka, koo husambaratika !

 

Si cha maji kitunguu, na saumu sijakuwa,

Nazihofu dafrau, za siasa na kuzua,

Naitafuta nafuu, penye ukiwa kukaa,

Tambiko likiondoka, koo husambaratika !

 

Nawaachia ukuu, waliobeba dunia,

Mimi naenda sahau, yote nikayaachia,

Nikahifadhi nahau, wajukuu kuzijua,

Tambiko likiondoka, koo husambaratika !

 

Namshukuru Afuu, hapo nilipofikia,

Mukubuli nanukuu, yake nimeyaridhia,

Naendeleza juzuu, daraja nende patiwa,

Tambiko likiondoka, koo husambaratika !

Wewe ukishakipata

 
Ndivyo ilivyo dunia, watu huipigania,
Na wanachopigania, hamu ikawaishia,
Wakishakujipatia, tafrani zikapoa,
Wewe ukishakipata, changamoto hupotea!
 
Husumbuka na dunia, bilkuli kuwania,
Kwa linalowazuzua, mfukoni kulitia,
Hamadi likitulia, ari inadidimia,
Wewe ukishakipata, changamoto hupotea!
 
Mbio watazitimua, nyikani wakapotea,
Marathoni mara kuwa, ovyo wanajihemea,
Ila wakiambulia, hurudi wakatulia,
Wewe ukishakipata, changamoto hupotea!
 
Hutamani ya dunia, na wao kujipatia,
Mikononi wakitia, hawa inawaishia,
Jingine kuangalia,wapi la kulifuatia,
Wewe ukishakipata, changamoto hupotea!
 
Hutetemesha jamaa, hadi wakamchukia,
Na dharau kuzitoa, vishindo akavitia,
Akatingisha dunia, tunda kwenda liangua,
Wewe ukishakipata, changamoto hupotea!
 
Likija mdondokea, kudaka huparamia,
Kisha akachuchumia, mikononi kulitia,
Anapoliangalia, si dhahabu akajua,
Wewe ukishakipata, changamoto hupotea!