Monday, January 28, 2013

UNACHOKITEGEMEA


Kinaweza kupotea, tena kutokujionea,

Ukabakia mkiwa, daima wewe kulia,

Na kurudi sio njia, huyoyoma na kwishia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Leo unakiringia, kesho utakililia,

Kisha ukaugilia, asante hukuitoa,

Shere ulikichezea, na dosari kukitia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Ujivuni ukavia, na kukushuka kifua,

Haya ukaisikia, wengi ulivyonyanyapaa,

Ukajuta kwa kinaya, tena hutojionea,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Wote uliowaambaa, hutamani kurejea,

Na wasiojitambua, mtego wataingia,

Ila kwa wenye kujua, mbali sana watakaa,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Nafasi hukuachia, upate vema pumua,

Njia wakaifagia, pasina kuitumia,

Milango wakifungua, ndani patupu pakawa,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Macho watayachezea, kama makengeza kuwa,

Na duara kuyatia, kama Kipanya wakawa,

Mchoro ukaujua, ni katuni maridhiwa,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Katika hii dunia, hupewa na hutwaliwa,

Tayari unapokaa, hili utaling'amua,

Vyote aushi si nia, huja vikajiondokea,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Nipe ridhiko Jalia, kwa kuwa na kutokuwa,

Ikawa kwa historia, utawa ninaujua,

Ubora uliokuwa, ni kwa vyote kuachia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Nisiwe wa kubomoa, patakapo kukamua,

Jiwe kutokaribia, maziwa halitatoa,

Katiti nilichopewa, nizidi kuangalia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Nisiwe kung'ang'ania, pale nisipotakiwa,

Kila anayechanua, thamani hujikuzia,

Sina la kuongezea, siidanganyi dunia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Hapo nilipofikia, mbele sintoendelea,

Yangu yamehasabiwa, zaidi haitakuwa,

Mwalimu niliyekuwa, mwanafunzi ninakuwa,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

 

Naenda tafuta njia, upenyoni kupitia,

Nusura kuifichua, tunduni iliokotiwa,

Mimi nikaichukua, mkononi kuitia,

Unachokitegemea, kinaweza kupotea!

No comments: