Monday, August 26, 2013

BARUA


Barua nimepokea, pasina kujitambua,
Jina nishaling'amua, langu wala haikuwa,
Maudhui nashangaa, ni jambo nisilojua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Raha nilijisikia, namiye kuandikiwa,
Japo sikumtambua, aliyeniandikia,
Kusoma nikajitia, kwa juhudi kuuvmbua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Wallahi sikudadavua, wala kitu kutambua,
Ila nimechanganyikiwa, asili nisiyoijua,
Na sasa najiinamia, kuwaza na kuwazua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Dhamira sijaijua, wala lililokusudiwa,
Lengo sijalitambua,  ramli sikujaliwa,
Kichwa ninaugulia, yote nataka kujua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Utata unenijaa, nasibu  naichezea,
Geresha ingelikuwa, nia sijaitambua,
Mengine kuyang'amua, subira yahitajiwa,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Mwanga ninaungojea, hili kuja niangazia,
Pengine nitagundua, japo palipoanzia,
Kisha nikaendelea, kufuma na kufumua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

MTU MWEMA

Shetani keshajitoma, ndaniyo ametulia,
Dhamiri tokea zama, yako kkutibulia,
Ukaikimbia njia, ya uzima pia twaha,
Mtu mwema kumuiza, huhamia ibilisi !

Shetani akuhadaa, kuona bora dunia,
Sasa wamtumikia, pasina kujitambua,
Serikali ilokuwa, Mola inamkataa,
Mtu mwema kumuiza, huhamia ibilisi !

Shere inamfanzia, aliyeumba dunia,
Wao juu wamekuwa,  na uchungi wakataa,
Milango waiachia, ibilisi kujimwaa,
Mtu mwema kumuiza, huhamia ibilisi !

Mtu tunamhofia, Mola tunamchezea?
Subira kaichagua, twasema amefulia ?
Yaja tusiyoyajua, kizazi tualilia,
Mtu mwema kumuiza, huhamia ibilisi !

Ibada twazikimbia,  sherehe kuziwania,
Muda ametuachia, tawba kuirejea,
Unguja na Tanzania, huruma ninawaonea,
Mtu mwema kumuiza, huhamia ibilisi !

Kitabu twakitania, na dini kuifukia ?
Kati yetu sijajua, nani alokuwa juha,
Ya miezi twaridhia, ya karne twaachia?
Mtu mwema kumuiza, huhamia ibilisi !

JIPENDELEE


NI kama soko dunia, huwezi vyote nunua,
Nawe unapojaliwa, kapu umelichukua,
Utakacho kuchukua, pengine kitakufaa,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Na unachokujakuwa, mimi siwezi nikawa,
Njia tunazopitia, kamwe sawa hazitakuwa,
Na nitapopumzikia, wewe hautapajua,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Njiani tullikutania, ndipo tulipoishia,
Itabaki kusikia,  pengine kujionea,
Ila pamoja kukaa, tena haitatokea,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Pamoja tulipokaa, na furaha kuijua,
Fursa tukatumia, nafsi kuziridhia,
Simulizi hubakia, hadi kujiondokea,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Pendo tuliloadhia, ukaribu ulizua,
Kweli tukaidhania, kumbe ashiki zakoa,
Sura zilipopotea, hamu zikajifia,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Na hiyo ndiyo dunia, mambo inayoyazua,
katikati hujifia, kustawi haitakuwa,
Unabakia umbeya, na mengi ya kusikia,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 


MWENYEZI MUNGU HASHINDWI

WALE wanaodhania, eti Mungu kafulia,
Wangejirudi tabia, subira wakatumia,
Yake keshajipangia, vipi unampangia?
Twapishana kwa wakati, Mwenyezi Mungu hashindwi!

Sivyo anavyoamua, kwa unavyofikiria,
Haendi kwa hatua, unazomhesabia,
Kumi ukijipangia, yeye elfu hutimia,
Twapishana kwa wakati, Mwenyezi Mungu hashindwi!

Subira jina kapewa, mcheleweshaji dunia,
Hatraka akimua, huibadili dunia,
Vikwazo akivitoa, na urahisi kwingia,
Twapishana kwa wakati, Mwenyezi Mungu hashindwi!

PIa aweza amua, ugumu ukaingia,
Kila mnalolifungua, ikawa linakataa,
Hata girisi kitia, bawaba hung'ang'ania,
Twapishana kwa wakati, Mwenyezi Mungu hashindwi!

Majinuni huugua, kweli wakaikataa,
Imani huwaishia, ukafiri kurejea,
Wakawa si wa kusikia, hadi kiyama kwingia,
Twapishana kwa wakati, Mwenyezi Mungu hashindwi!

Mola unayetujua, tasihirili twlailia,
Mioyo kuiridhia, kubuli ikshaingia,
Vingine kutoshania, ili tu kukutegema,
Twapishana kwa wakati, Mwenyezi Mungu hashindwi!

AFAAYE UONGOZI

Sio mtu wa sanaa, wala wa kuionesha,
Ni mja wa kujitambua, mengi anayeng'amua,
Na uchamungu ajua, tawba akaililia,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!

Ukubwa atahofia, asije akakosea,
Dhamanaye aijua, ya akhera na dunia,
Humuogopa Jalia, asije kumkosoa,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!

Ukubwa huuridhia, akishaiona njia,
Fakiri kusaidia, na zaka kuichangia,
Yawe yanayowafikia, wale waliokusudiwa,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!

Ukubwa hautauvaa, kama vile ni kofia,
Watu kumshangilia, na vigelegele kulowa,
Mate akasimbuliwa, na najisi kuchukua,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!

Huwa wa kuelekea, ukweli anaoujua,
Hasira kuzihofia, zisije mwangukia,
Kwani ajua dunia, hii ni ya mpito njia,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!

Lengo atajiwekea, la hesabu kutimia,
Pasina kitu kupungua, siku itapowadia,
Lulu alizoahidiwa, asije mwingine pewa,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!

Kazi anajichapia, ukubwa hatofikiria,
Wenye shida kutatua, wala si kuwanunua,
Uovu akafagia, nchi safi kubakia,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!
Zama alikusudiwa, marehemu angekuwa,
Ubaya aliofanyiwa, kwake dawa kuja kuwa,
Mola mwingi wa nazaa, na hadaa azijua,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!

CHA BURE KINGINE GHALI


Humuachia amali, ajuaye jipangia,
Fahari kuwa fahali,  dongo lililoumbwa,
Akasema kwa mithali, mjinga hujibomoa,
Sasa nimeshatambua, rahisi nyingine ghali !

Rahisi nyingine ghali, mwanangu nakuambia,
Ikubali idhilali, kidogo kuongezea,
Ukajitoa muhali, ili kesho kukufaa,
Sasa nimeshatambua, rahisi nyingine ghali !

Mbishi hatokubali, bei atapigania,
Kwa kutojua ukweli, aali akakosea,
Muuza akijakubali, thamani keshapangua,
Sasa nimeshatambua, rahisi nyingine ghali !

Huzigundua dalili, haki hatoiridhia,
Kwa kuondoa idhilali, yeye huyakubalia,
Kwisha kuwa kulhali, maisha yakaendelea,
Sasa nimeshatambua, rahisi nyingine ghali !

Haambiliki anzali, huna la kumuelezea,
Hudhani astahili, daima ni kusifiwa,
Akakataa kubuli, na hadaa kununua,
Sasa nimeshatambua, rahisi nyingine ghali !

Humuachia amali, ajuaye jipangia,
Fahari kuwa fahali,  dongo lililoumbwa,
Akasema kwa mithali, mjinga hujibomoa,
Sasa nimeshatambua, rahisi nyingine ghali !

MWENYYE THAMANI


Wengine wa kutumiwa, kwa azijuazo ndia,
Kwa ndogo na kubwa gia,yeye  keshajipangia,
Yote keshakadiria, thamani kajipangia,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!

Kiasi anakijua, kaishawahesabia,
Wagawaji kachagua, vibaba kwenda vitoa,
Kikubwa kinachobakia, kuwadi watapatiwa,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!

Kama shehe anajua, firdausi katwaa,
Kasri keshajipangia, huko aenda ingia,
Bawabu watamjua,  wakati keshaingia,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!

Mbawa atajiotea, na mbinguni akapaa,
Akaicheka dunia, ubora alishajaliwa,
Daraja akatumia, ya kwake kuyaamua,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!

Huiba akafidia, kule kulikopungua,
Asopendwa huonewa, kidogo kutoachiwa,
Mbavu wakazikazia, dhiki kumshambulia,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!

Ila wanaomsifia, karamu watafanziwa,
Vitu kuteremshiwa, hata wasivyofikiria,
Ipambwe yao dunia, mauti  kuyatania,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!