Monday, August 26, 2013
MWENYYE THAMANI
Wengine wa kutumiwa, kwa azijuazo ndia,
Kwa ndogo na kubwa gia,yeye keshajipangia,
Yote keshakadiria, thamani kajipangia,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!
Kiasi anakijua, kaishawahesabia,
Wagawaji kachagua, vibaba kwenda vitoa,
Kikubwa kinachobakia, kuwadi watapatiwa,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!
Kama shehe anajua, firdausi katwaa,
Kasri keshajipangia, huko aenda ingia,
Bawabu watamjua, wakati keshaingia,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!
Mbawa atajiotea, na mbinguni akapaa,
Akaicheka dunia, ubora alishajaliwa,
Daraja akatumia, ya kwake kuyaamua,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!
Huiba akafidia, kule kulikopungua,
Asopendwa huonewa, kidogo kutoachiwa,
Mbavu wakazikazia, dhiki kumshambulia,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!
Ila wanaomsifia, karamu watafanziwa,
Vitu kuteremshiwa, hata wasivyofikiria,
Ipambwe yao dunia, mauti kuyatania,
Kila mtaka ukubwa, mwenye thamani ni yeye!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment