Monday, August 26, 2013

BARUA


Barua nimepokea, pasina kujitambua,
Jina nishaling'amua, langu wala haikuwa,
Maudhui nashangaa, ni jambo nisilojua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Raha nilijisikia, namiye kuandikiwa,
Japo sikumtambua, aliyeniandikia,
Kusoma nikajitia, kwa juhudi kuuvmbua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Wallahi sikudadavua, wala kitu kutambua,
Ila nimechanganyikiwa, asili nisiyoijua,
Na sasa najiinamia, kuwaza na kuwazua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Dhamira sijaijua, wala lililokusudiwa,
Lengo sijalitambua,  ramli sikujaliwa,
Kichwa ninaugulia, yote nataka kujua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Utata unenijaa, nasibu  naichezea,
Geresha ingelikuwa, nia sijaitambua,
Mengine kuyang'amua, subira yahitajiwa,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

Mwanga ninaungojea, hili kuja niangazia,
Pengine nitagundua, japo palipoanzia,
Kisha nikaendelea, kufuma na kufumua,
Barua uliyotuma, haikuwa na anwani !

No comments: