Sio mtu wa sanaa, wala wa kuionesha,
Ni mja wa kujitambua, mengi anayeng'amua,
Na uchamungu ajua, tawba akaililia,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!
Ukubwa atahofia, asije akakosea,
Dhamanaye aijua, ya akhera na dunia,
Humuogopa Jalia, asije kumkosoa,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!
Ukubwa huuridhia, akishaiona njia,
Fakiri kusaidia, na zaka kuichangia,
Yawe yanayowafikia, wale waliokusudiwa,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!
Ukubwa hautauvaa, kama vile ni kofia,
Watu kumshangilia, na vigelegele kulowa,
Mate akasimbuliwa, na najisi kuchukua,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!
Huwa wa kuelekea, ukweli anaoujua,
Hasira kuzihofia, zisije mwangukia,
Kwani ajua dunia, hii ni ya mpito njia,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!
Lengo atajiwekea, la hesabu kutimia,
Pasina kitu kupungua, siku itapowadia,
Lulu alizoahidiwa, asije mwingine pewa,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!
Kazi anajichapia, ukubwa hatofikiria,
Wenye shida kutatua, wala si kuwanunua,
Uovu akafagia, nchi safi kubakia,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!
Zama alikusudiwa, marehemu angekuwa,
Ubaya aliofanyiwa, kwake dawa kuja kuwa,
Mola mwingi wa nazaa, na hadaa azijua,
Afaaye uongozi, dhima huwa akimbia!
Monday, August 26, 2013
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment