Monday, August 26, 2013

JIPENDELEE

NI kama soko dunia, huwezi vyote nunua,
Nawe unapojaliwa, kapu umelichukua,
Utakacho kuchukua, pengine kitakufaa,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Na unachokujakuwa, mimi siwezi nikawa,
Njia tunazopitia, kamwe sawa hazitakuwa,
Na nitapopumzikia, wewe hautapajua,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Njiani tullikutania, ndipo tulipoishia,
Itabaki kusikia,  pengine kujionea,
Ila pamoja kukaa, tena haitatokea,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Pamoja tulipokaa, na furaha kuijua,
Fursa tukatumia, nafsi kuziridhia,
Simulizi hubakia, hadi kujiondokea,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Pendo tuliloadhia, ukaribu ulizua,
Kweli tukaidhania, kumbe ashiki zakoa,
Sura zilipopotea, hamu zikajifia,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

Na hiyo ndiyo dunia, mambo inayoyazua,
katikati hujifia, kustawi haitakuwa,
Unabakia umbeya, na mengi ya kusikia,
Jipendelee mwenzangu, je, kutesa si kwa zamu? 

No comments: