Saturday, May 5, 2012
KIswahili kinazikwa
Watu wamenunuliwa, Kiswahili kukiua,
Ujanja wanatumia, wengine kuwahadaa,
Kumbe wao kulemaa, ndio wanakazania,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Ugiriki walikuwa, wa kwanza kwenye dunia,
Elimu kupalilia, mengi tusiyoyajua,
Hadi leo tunajua, mema yaliyozaliwa,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Ila walihadaiwa, dharau ikawajaa,
Lugha wakapuuzia, Kilatini kuingia,
Walipokujashtukia, marehemu imekuwa,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Walipokujashtukia, marehemu imekuwa,
Kimataifa yapwaya, ngumu kujaheshimiwa,
Uzito imepungua, ukimwi kuiingia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Kilatini nacho pia, siku kilipozainiwa,
Wasomi wakajitia, tajiri tu wanafaa,
Na wakubwa walokuwa, lugha hiyo kuijua,
Walipokujashtukia, marehemu imekuwa,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Masikini kuambiwa, kubwa kwao imekuwa,
Hawafai kuijua, haitowasaidia,
Kumbe imehukumiwa, kaburini kuingia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Zipo nyingi lugha pia, katika hii dunia,
Wakubwa walipopwaya, ulinzi wakaachia,
Mageni kukumbatia, madawa yakawalevya,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Na pale walipolewa, lugha zao kujifia,
Ni watumwa wamekua, inawacheka dunia,
Laiti wangelijua, haya yasingetokea,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Yatufunza historia, lugha uwezavyo kuua,
Hapa kwetu Tanzania, ndicho sasa chatokea,
Bungeni imefikia, wauangaji waingia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Laana nawaombea, mema wasiyoitakia,
Ianze kwao kutua, na kizazi kufatia,
Kama wakija kuua, lugha yetu asilia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Masikini mwatakiwa, lugha yenu kutetea,
Kwa uchumi imejaa, si fukara nawambia,
Ila wasiojaliwa, udni wanatutia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Kiswhili mashalaa, kutawala kinafaa,
Tena sio Tanzania, hata pia na dunia,
Kiarabu kimejaa, themanini yake mia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Kiarabu kimejaa, thamania asilimia,
Kama chaweza wafaa, kwanini sisi kuvia,
Ila tumelogewa, wanyonyaji kutunywea?
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Hasira nimeitia, na kweli nawaambia,
Viongozi walokuwa, dhambi wametufanyia,
Na alam tutatia, Kiswahili waliua,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
KIONGOZI maridhia, kuenziwa Tanzania,
Lugha atakayeamua, Kiswahili kutumiwa,
Wengi wapate jaliwa, elimu kuendelea,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Wengi wapate jaliwa, elimu kuendelea,
Lugha wakifundishiwa, hadi daktari kuwa,
Ikiwa wanaridhia, nyingine watazijua,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Ikiwa wataridhia, nyingine watazijua,
Tena wawe wachagua, na sio kuamriwa,
Kiarabu kikifaa, basi wataendelea,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Kiarabu kikifaa, hiyo sawa itakuwa,
Kichina chafaa pia, maabara wataingia,
Huko watajisomea, hata pia lugha mia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Lakini kuendelea, chetu tutakitumia,
Hadi tafiti kutia, wenyewe kuzitumia,
Siri tukajitunzia, sio kila mtu kutujua,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Mapeni wamechukua, Mwingereza kuyatoa,
Mfukoni wakatia, lugha yetu kuiua,
Na uzungu kujitia, lipi wanalolijua?
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Hebu sasa angalia, Uchina imeshapaa,
Na India nayo pia, juu juu waelea,
Kisa yao kutumia, na si cha kung'ang'aniwa,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Yarabi nakulilia, lugha kutuhifadhia,
Waovu kutowaachia, wasije wakakiua,
Kije sisi kutufaa, na vizazi vyetu pia,
Kiswahili kinazikwa, na sisi twaangalia?
Ndugu zetu Waarabu
Nimekuja kugundua, ahali sikuwajua,
Ila walotulalia, akili kutuchezea,
Hadi kuwaabudia, na sasa tunapotea,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Damu nimeigundua, kila pembe yaenea,
Dini waliichukia, mpya na asilia,
Nasara wakavamia, athari kuziondoa,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Ila hawakujaliwa, ulinzi umebakia,
Mwenyewe kaangalia, hadi leo kufikia,
Haifai kumwachia, uamsho watakiwa,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Hapa linalokusudiwa, dini yetu kurejea,
Huku tunajitambua, Kiswahili tulipewa,
Vyama tukikitumia, mbali sana tutapaa,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Vyuo mnangojewa, kuja kujianzishia,
Elimu ikaitoa, kwa lugha pacha zikawa,
Kiswahili na Arabia, tulivyokwishajaliwa,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Vyuo vikuu pia, lugha kuzifundishia,
Hadi dokta wakawa, ndugu zetu Tanzania,
Na kisha kufuatia, Afrika ikapaa,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Themanini kwayo mia, ni yake asilimia,
Maneno Kiarabia, Kiswahii imetwaa,
Hili ukizingatia, lugha kujua inafaa,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Gele wanatuonea, Wahausa Nigeria,
Kama wao wangekuwa, hatua wangeshachukua,
Na mazuri yakajaa, na wala sio balaa,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Kitu hatujapungukiwa, yabaki kuzitumia,
Unyonge tukajivua, na asili kuringia,
Kiingereza kitapwaya, wallahi nawaambia,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Ndugu zetu twawajua, umoja tunatakiwa,
Yetu kuja fanikiwa, kitu kimoja i dua,
Vingine tukiachia, lazima tutahujumiwa,
Ndugu zetu Waarabu, na wala sio wazungu !
Rafiki zetu Wachina
Kasumba yatuhadaa, magharibi kwangalia,
Mugabe keshatwambia, nyakati zimefikia,
Mashariki kuingia, rahisi kukubaliwa,
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !
Funguo za kuendelea, Magharibi zafulia,
Asia ndiko kwafaa, kuuza na kununua,
Hamuoni yatokea, au vipogu mmekua?
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !
Wachina tunawajua, mengi wametusaidia,
Akili tukijaliwa, hawa kuwashikilia,
Mengi watatupatia, kielimu tukajua,
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !
Treni walitujengea, kwanini kutofufua,
Meli wanajiundia, na magari nayo pia,
Hata ndege wanajua, sio tena kununua,
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !
Kompyuta wazifua, na simu wajiundia,
Sawasawa tukiingia, yote haya twajivunia,
Sisi tunawakimbia, kwingine kuwaendea ?
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !
Tunazifata hadaa, na wajanja walokuwa,
Waliozusha balaa, wakaiumiza dunia,
Na Mungu kumshukia, watu wake wakaua?
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !
Mola tunamshtakia, hukumu yake kutoa,
Wanaotung'ang'anizia, mbali sana kutofikia,
Mapema kuwaumbua wakweli tukachagua,
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !
Qatar onyesha njia
Qatar nawasifia, Aljazeera tangazia,
Milango mwaifungua, nchi zetu kuendelea,
Wazungu watuhadaa, shere wanatuchezea,
Qatar onyesha njia, wengine wafuatia !
Ugonjwa wanaujua, pia dawa waijua,
Ni sisi kuwaingia, wapate tusaidia,
Macho watatufungua, mengi sana kuyajua,
Qatar onyesha njia, wengine wafuatia !
Uchumi tumekalia, wazungu watuchezea,
Pipi wanatuigaia, dhahabu twawaachia,
Ujinga tumejaliwa, si mdogo ulokuwa,
Qatar onyesha njia, wengine wafuatia !
Ninakuomba Jalia, hili kuliangalia,
Wema kutuchagulia, wakaweza kutufaa,
Na udugu kuungia, walio na manufaa,
Qatar onyesha njia, wengine wafuatia !
Lengo kuu kidunia
Imepwaya jumuiya, katika hii dunia,
Ovyoovyo twatembea, hata haramu kuvua,
Na kila ukiangalia, dini tunaichezea,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Angalia Tunisia, huko yaliyotokea,
Kisha ikafuatia, ya Gaddafy Libya,
Masri na Syria, sasa yanaendelea,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Kwingineko Indonesia, nako pia Malaysia,
Na zile za Kijamaa, Urussi zilizokua,
Kila ukiangalia, madhambi yawazidia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Uchamungu wafulia, kisha bado wanalia,
Machafu wayaachia, nchini yanaingia,
Neema wazikataa, mgeni kuabudia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Nasi tulishaambiwa, Miungu yao kuwaachia,
Wetu mmoya radhia, Azizi kuabudia,
Shiriki aikataa, na hili tunalijua,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Trela yaendelea, sinema haijaanzia,
Tsunami zaingia, kwa kushsto na kulia,
Na mioto naiwazia, siku ikijafikia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Mengi sana yatavia, ukame ukijatokea,
Na kisa kuabudiwa, watu wanaozaliwa,
Tukaacha jitambua, Muumba kumhofia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Iko siku tutalia, sio mbali nadhania,
Ukame ukiingia, na njaa ikasambaa,
Kisiote cha kufaa, na wanyama kujifia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Viongozi wayajua, waliokijifanyia,
Hawana wa kusingizia, hukumu ikiwadia,
Ukimya waliokaa, hofu nyingi wanitia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Ukimya waliokaa, hata wale wa dini pia,
Siwezi kuja shangaa, adhabu ikizidia,
Na mimi kusamehewa, sithubutu kujiombea,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Ni mmoja nimekuwa, kwa kushindwa kujijua,
Mapema ningewaambia, labda mngefikiria,
Makosa ninatubia, afu siwezi kataa,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !
Hivi vyote vya dunia
Hivi vyote vya dunia, huanza na kuishia,
Na wanaozuzuliwa, kubaya waelekea,
Muda ukishawadia, hana la kujitetea,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Vitu vinatuzuzua, na watu watununua,
Hadhi yetu kitumbua, ughali hatujaujua,
Sinema yetu dunia, kwingine hatujaangalia,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Ombwe tunapigania, kesho lisilotufaa,
Na madeni twanunua, tena kwa kujiaminia,
Siku hiyo kuyavua, mbona kazi itakuwa,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Majumba twayalilia, japo ukweli twajua,
Kaburi haitakuwa, mita mraba kadhaa,
Huko kwa sana kukaa, hadi kuja fufuliwa,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Magari twakimbilia, kumbe twaenda jiua,
Vikorokoro vyajaa, hata visivyotufaa,
Kila ukiangalia, naona hatujajijua,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Shughuli twafatilia, thawabu zisikotiwa,
Na mengi kushangilia, yakuja kuugulia,
Siku iwe waangalia, huku unajililia,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Ukweli twauhadaa, uongo twashikilia,
Islamu wabaya, watu wanatuhofia,
Na wengine walokuwa, ndugu wanawazulia,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Twatendeana ubaya, kamab tumeiachia,
Unafiki wachanua, kila kona wajiotea,
Na dini yahujumiwa, na wanaonunuliwa,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Kisirani imekua, maabadi yahofiwa,
Waweza kulipuliwa, mbali ukajifilia,
Na hii siyo hidaya, ni laana nahofia,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Hakuna aliye mbora
Hakuna aliye bora, ila mwenye ucha Mungu,
Zenu kukuru kakara, mwisho wake ni mawingu,
Mawazo ya kifukara, yanawatia kiwingu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!
Kwanini mnadorora, mwaishia ya mvungu,
Hazifani zenu sura, hudhani mwapigwa rungu,
Yawaishia stara, kwa kuzunguka mizungu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!
Na wanaojiona bora, sawasawa na mabungu,
Hupaa kwenye ziara, wakirudi ni utungu,
Huishia kudorora, wakayakumba machungu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!
Nayaomba maghufira, ukumbi huu si wangu,
Sijaiona bishara, kupata mradi wangu,
Nami si mwenye kuchora, nikala hata vya wenzangu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!
Naikubali kudura, haya i usoni mwangu,
Kama chungu ninagura, na wangu pia mkungu,
Na wala sina harara, hulingoja langu fungu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!
Ufukara wa mawazo
Ni mkubwa umasikini, kama fedha huna ndani,
Ila mie naamini, upo nisioutamani,
Na huu sio mgeni, naanika hadharani,
Ufukara wa mawazo, hakika unanitisha !
Siogopi umaskini, wala sijioni duni,
Ila niko mashakani, pasipo kitu kichwani,
Hujiona hayawani, na wala sijithamini,
Ufukara wa mawazo, hakika unanitisha !
Unatisha kwa yakini, wa mawazo umaskini,
Huwa kama afkani, taahirra majinuni,
Mtu huwezi jiamini, daima kuwa taabani,
Ufukara wa mawazo, hakika unanitisha !
Nauogopa amini, na katu siutamani,
Bora kingine yakini, huwa kwangu uhaini,
Nitakimbia jangwani, iwe watu siwaoni,
Ufukara wa mawazo, hakika unanitisha !
Usikatishe udugu
Udugu usikatishe, kwa kutokuelewana,
Damu msiikatishe, eti tu kwa kuzozana,
Kufaana msiishe, mtakuja kumbukana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!
Mwenzie umsemeshe, hata mnapogombana,
Kisha basi na yaishe, na radhi mkatakana,
Udugu msikatishe, hilo hapendi Rabana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!
Pengine mgonganishwe, na wagomvi wenu wa jana,
Ya uongo wayazushe, ili nyie mkagombana,
Haiwi mjjikaushe, haya mkaja yaona,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!
Watu wasiwawabaishe, nyie budi kuzikana,
Hata wawagombanishe, budi kuja elewana,
Acheni wakorofishe, yao kwao kutofichana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!
Hadharani msibishe, waacheni kutoona,
Na nyie mjivishe, kama nanyi ni watwana,
Waacheni nje wakeshe, huku yenu mwayabana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!
Nendeni mjipumzishe, msije kuumizana,
Na pumzi mzishushe, shetani kuondokana,
Huja vurugu ziishe, na ndugu mkaelewana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!
Usiue urafiki
Sababu ya kosa moja, unaua urafiki,
Naona hiyo si hoja, au wacheza falaki,
Rafiki kubwa daraja, rahisi halibomoki,
Usiue urafiki, sababu ya kosa moja !
Ungeufunga mkaja, ujue lipi ni haki,
Na maneno ya waseja, haiwi yo yake laki,
Sahihi linalokuja, kuijali tawfiki,
Usiue urafiki, sababu ya kosa moja !
Ndio rojo yenye koja, haitaki unafiki,
Hainyewi kwa mrija, mdomo ndiyo yake haki,
Hakika mbili si moja, vingine haiaminiki,
Usiue urafiki, sababu ya kosa moja !
Subscribe to:
Posts (Atom)