Saturday, May 5, 2012

Rafiki zetu Wachina

Kasumba yatuhadaa, magharibi kwangalia,
Mugabe keshatwambia, nyakati zimefikia,
Mashariki kuingia, rahisi kukubaliwa,
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !

Funguo za kuendelea, Magharibi zafulia,
Asia ndiko kwafaa, kuuza na kununua,
Hamuoni yatokea, au vipogu mmekua?
 Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !

Wachina tunawajua, mengi wametusaidia,
Akili tukijaliwa, hawa kuwashikilia,
Mengi watatupatia, kielimu tukajua,
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !

Treni walitujengea, kwanini kutofufua,
Meli wanajiundia, na magari nayo pia,
Hata ndege wanajua, sio tena kununua,
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !

Kompyuta wazifua, na simu wajiundia,
Sawasawa tukiingia, yote haya twajivunia,
Sisi tunawakimbia, kwingine kuwaendea ?
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !

Tunazifata hadaa, na wajanja walokuwa,
Waliozusha balaa, wakaiumiza dunia,
Na Mungu kumshukia, watu wake wakaua?
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !

Mola tunamshtakia, hukumu yake kutoa,
Wanaotung'ang'anizia, mbali sana kutofikia,
Mapema kuwaumbua wakweli tukachagua,
Rafiki zetu Wachina, na wala sio wazungu !

No comments: