Saturday, May 5, 2012

Usikatishe udugu




Udugu usikatishe,  kwa kutokuelewana,
Damu msiikatishe, eti tu kwa kuzozana,
Kufaana msiishe, mtakuja kumbukana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!

Mwenzie umsemeshe, hata mnapogombana,
Kisha basi na yaishe, na radhi mkatakana,
Udugu msikatishe, hilo hapendi Rabana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!

Pengine mgonganishwe, na wagomvi wenu wa jana,
Ya uongo wayazushe, ili nyie mkagombana,
Haiwi mjjikaushe, haya mkaja yaona,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!

Watu wasiwawabaishe, nyie budi kuzikana,
Hata wawagombanishe, budi  kuja elewana,
Acheni wakorofishe, yao kwao kutofichana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!

Hadharani msibishe, waacheni  kutoona,
Na nyie mjivishe, kama nanyi ni watwana,
Waacheni nje wakeshe, huku yenu mwayabana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!

Nendeni mjipumzishe, msije kuumizana,
Na pumzi mzishushe, shetani kuondokana,
Huja vurugu ziishe, na ndugu mkaelewana,
Usikatishe udugu, kwa kutokuelewana!

No comments: