Saturday, May 5, 2012

Hakuna aliye mbora



Hakuna aliye bora, ila mwenye ucha Mungu,
Zenu kukuru kakara, mwisho wake ni mawingu,
Mawazo ya kifukara, yanawatia kiwingu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!

Kwanini mnadorora, mwaishia ya mvungu,
Hazifani zenu sura, hudhani mwapigwa rungu,
Yawaishia stara, kwa kuzunguka mizungu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!

Na wanaojiona bora, sawasawa na mabungu,
Hupaa kwenye ziara, wakirudi ni utungu,
Huishia kudorora, wakayakumba machungu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!

Nayaomba maghufira, ukumbi huu si wangu,
Sijaiona bishara, kupata mradi wangu,
Nami si mwenye kuchora, nikala hata vya wenzangu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!

Naikubali kudura, haya i usoni mwangu,
Kama chungu ninagura, na wangu pia mkungu,
Na wala sina harara, hulingoja langu fungu,
Hakuna aliye mbora, zaidi ya Mchamungu!

No comments: