Saturday, May 5, 2012

Qatar onyesha njia



Qatar nawasifia, Aljazeera tangazia,
Milango mwaifungua, nchi zetu kuendelea,
Wazungu watuhadaa, shere wanatuchezea,
Qatar onyesha njia, wengine wafuatia !

Ugonjwa wanaujua, pia dawa waijua,
Ni sisi kuwaingia, wapate tusaidia,
Macho watatufungua, mengi sana kuyajua,
Qatar onyesha njia, wengine wafuatia !

Uchumi tumekalia, wazungu watuchezea,
Pipi wanatuigaia, dhahabu twawaachia,
Ujinga tumejaliwa, si mdogo ulokuwa,
Qatar onyesha njia, wengine wafuatia !

Ninakuomba Jalia, hili kuliangalia,
Wema kutuchagulia, wakaweza kutufaa,
Na udugu kuungia, walio na manufaa,
Qatar onyesha njia, wengine wafuatia !

No comments: