Saturday, May 5, 2012
Hivi vyote vya dunia
Hivi vyote vya dunia, huanza na kuishia,
Na wanaozuzuliwa, kubaya waelekea,
Muda ukishawadia, hana la kujitetea,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Vitu vinatuzuzua, na watu watununua,
Hadhi yetu kitumbua, ughali hatujaujua,
Sinema yetu dunia, kwingine hatujaangalia,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Ombwe tunapigania, kesho lisilotufaa,
Na madeni twanunua, tena kwa kujiaminia,
Siku hiyo kuyavua, mbona kazi itakuwa,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Majumba twayalilia, japo ukweli twajua,
Kaburi haitakuwa, mita mraba kadhaa,
Huko kwa sana kukaa, hadi kuja fufuliwa,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Magari twakimbilia, kumbe twaenda jiua,
Vikorokoro vyajaa, hata visivyotufaa,
Kila ukiangalia, naona hatujajijua,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Shughuli twafatilia, thawabu zisikotiwa,
Na mengi kushangilia, yakuja kuugulia,
Siku iwe waangalia, huku unajililia,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Ukweli twauhadaa, uongo twashikilia,
Islamu wabaya, watu wanatuhofia,
Na wengine walokuwa, ndugu wanawazulia,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Twatendeana ubaya, kamab tumeiachia,
Unafiki wachanua, kila kona wajiotea,
Na dini yahujumiwa, na wanaonunuliwa,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Kisirani imekua, maabadi yahofiwa,
Waweza kulipuliwa, mbali ukajifilia,
Na hii siyo hidaya, ni laana nahofia,
Hivi vyote vya dunia, vina mwanzo, vina mwisho!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment