Saturday, May 5, 2012

Lengo kuu kidunia



Imepwaya jumuiya, katika hii dunia,
Ovyoovyo twatembea, hata haramu kuvua,
Na kila ukiangalia, dini tunaichezea,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Angalia Tunisia, huko yaliyotokea,
Kisha ikafuatia, ya Gaddafy Libya,
Masri na Syria, sasa yanaendelea,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Kwingineko Indonesia, nako pia Malaysia,
Na zile za Kijamaa, Urussi zilizokua,
Kila ukiangalia, madhambi yawazidia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Uchamungu wafulia, kisha bado wanalia,
Machafu wayaachia, nchini yanaingia,
Neema wazikataa, mgeni kuabudia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Nasi tulishaambiwa, Miungu yao kuwaachia,
Wetu mmoya radhia, Azizi kuabudia,
Shiriki aikataa, na hili tunalijua,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Trela yaendelea, sinema haijaanzia,
Tsunami zaingia, kwa kushsto na kulia,
Na mioto naiwazia, siku ikijafikia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Mengi sana yatavia, ukame ukijatokea,
Na kisa kuabudiwa, watu wanaozaliwa,
Tukaacha jitambua, Muumba kumhofia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Iko siku tutalia, sio mbali nadhania,
Ukame ukiingia, na njaa ikasambaa,
Kisiote cha kufaa, na wanyama kujifia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Viongozi wayajua, waliokijifanyia,
Hawana wa kusingizia, hukumu ikiwadia,
Ukimya waliokaa, hofu nyingi wanitia,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Ukimya waliokaa, hata wale wa dini pia,
Siwezi kuja shangaa, adhabu ikizidia,
Na mimi kusamehewa, sithubutu  kujiombea,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

Ni mmoja nimekuwa, kwa  kushindwa kujijua,
Mapema ningewaambia, labda mngefikiria,
Makosa ninatubia, afu siwezi kataa,
Lengo kuu kidunia, hatuna twababaika !

No comments: