Saturday, May 5, 2012
Ufukara wa mawazo
Ni mkubwa umasikini, kama fedha huna ndani,
Ila mie naamini, upo nisioutamani,
Na huu sio mgeni, naanika hadharani,
Ufukara wa mawazo, hakika unanitisha !
Siogopi umaskini, wala sijioni duni,
Ila niko mashakani, pasipo kitu kichwani,
Hujiona hayawani, na wala sijithamini,
Ufukara wa mawazo, hakika unanitisha !
Unatisha kwa yakini, wa mawazo umaskini,
Huwa kama afkani, taahirra majinuni,
Mtu huwezi jiamini, daima kuwa taabani,
Ufukara wa mawazo, hakika unanitisha !
Nauogopa amini, na katu siutamani,
Bora kingine yakini, huwa kwangu uhaini,
Nitakimbia jangwani, iwe watu siwaoni,
Ufukara wa mawazo, hakika unanitisha !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment